JPM awataja Makamba na Ngeleja, ‘Niliamua kuwasamehe’

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa ameshawasamehe wabunge wawili ambao ni January Makamba pamoja na William Ngeleja, kufuatia kusikika baadhi ya sauti zilizosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii zikimtukana na kumdhihaki.

Amesisitiza kuwa suala la kusamehe ni jambo kuu na la msingi na kusema kuwa ameamua kuwasamehe wabunge hao, kwakuwa aliwaona wameomba msamaha kwa dhati ya mioyo yao ukizingatia na yeye humuomba msamaha Mungu aliyemuumba.

”Mimi nakumbuka hivi karibuni kuna watu fulani walinitukana tukana wee, nikakaa nikajiridhisha kuwa sauti ni zao kwa asilimia mia moja, nikawa nakaa nafikiliaa nikasema hawa wakipelekwa kwenye kamati Kuu ya Siasa ya Chama, adhabu itakuwa ni kubwa, nikasema bora ninyamaze lakini wakajitokeza wawili wakaniomba msamaha nikasema nisipowasamehe nitabaki na majeraha makubwa moyoni mwangu, ambao ni Mheshimiwa January Makamba na William Ngeleja na niliwasamehe na kusahau,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ameyabainisha hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa wakandarasi, uliofanyika jijini Dar es salaam ambapo amewabainishia changamoto zilizopo kwa upande wao,  ikiwa ni pamoja na kuendekeza vitendo vya rushwa na kutokuwa na uthubutu wa kuomba tenda pindi zabuni zinapotolewa.

”Miongoni mwa changamoto hizo ni kutokuwa na umoja na ushirikiano miongoni mwa wakandarasi wa ndani hali inayopelekea mshindwe kupewa miradi mikubwa na kuendeleza vitendo vya rushwa ili mpate zabuni, mwaka jana nakumbuka tulitangaza mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Chamwino kwenda Mjini nilitegemea kabisa Km 20, zitaombwa na wakandarasi wazalendo wala hamkuomba, sasa hapo unaweza kujiuliza wakandarasi wazawa wa makampuni ya ndani hawajui kuomba kazi” amesema Rais Magufuli

Hata hivyo, rais Magufuli ameitaka Wizara ya Ujenzi pamoja na Bodi ya wakandarasi kuhakikisha wanazitafakari kwa kina changamoto zilizopo, ikiwemo kuzidisha ukali kwa wataalamu wanaoenda kinyume na maagizo, ikiwemo kuhakikisha wanawafutia usajili wakandarasi wasiokuwa waadilifu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad