BABAKOCHA Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems amesema kuwa anataka kuona timu yake inapata ushindi wa mabao kuanzia matatu hadi matano kwenye michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 walipokutana na JKT Tanzania katika mchezo wa kwanza Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Alhamisi iliyopita.
Katika mchezo huo, mabao ya Simba yalifungwa na Mnyarwanda, Meddie Kagere aliyefunga mawili kabla ya Athumani Miraji kuingia katika kipindi cha pili na kufunga moja.
Akizungumza na Championi Jumatatu, alisema licha ya vijana wake kucheza vizuri, lakini hakuridhishwa na idadi ya mabao waliyofunga kutokana na nafasi nyingi walizozipata za kufunga ambazo kama wangekuwa makini wangefunga mabao matano.
Aussems alisema kuwa tayari amekaa na washambuliaji wake Meddie Kagere, Deo Kan dana John Bocco kwa ajili ya kuzungumza nao na kikubwa aliwasisitiza kutumia kila nafasi watakazozipata katika mechi.
Aliongeza kuwa anataka kuona timu inapata ushindi wa mapema ndani ya dakika 15 za mwanzo mara baada ya mchezo kuanza kwa lengo la kuwavuruga wapinzani wao.
“Siku zote unapopata bao la mapema mpinzani wako anachanganyikiwa kwa kucheza kwa presha kubwa, hivyo nimewataka washambuliaji wangu kuongeza umakini wakiwa ndani na nje ya 18 kwa kutumia vema nafasi za kufunga.
“Kama unakumbuka mchezo wetu uliopita wa ligi tulipocheza na JKT, wachezaji wangu walitengeneza nafasi nyingiza kufunga kama wangekuwa makini, basi mchezo huo ungemalizika mapema, basi tungeibuka na ushindi wa mabao matano.
“Na hicho ndiyo kitu kinachokitaka kwani ushindi wa mabao mengi, mwishoni mwa ligi yatakuwa na faida kubwa kama ikitokea tukiwa na pointi sawa, ni matarajio yangu kuwaona wachezaji wakibadilika kwa haraka,” alisema Aussems.