HALI ya mambo kwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu ambaye amejiunga na timu hiyo hivi karibuni akitokea Yanga, sasa si shwari tena ndani ya kikosi cha timu hiyo.
Hali hiyo inatokana na kuvuliwa ufalme aliokuwa nao msimu uliopita wakati akiwa Yanga na kupewa kiungo mwingine mshambuliaji wa timu hiyo, Miraji Athumani ‘Sheva’ ambaye pia amejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Lipuli FC.
Akizungumza na Championi Jumatano, kocha wa zamani wa wachezaji hao, Seleman Matola alisema kuwa ni ngumu Ajibu kujifananisha na Sheva kwa sasa. Matola alisema kuwa Sheva ambaye juzi Jumatatu aliitwa katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars ni bora zaidi.
“Kwa jinsi ninavyomjua Sheva hakika yeye ndiye atakayekuwa bora kwa vijana wangu wote niliowafundisha katika kikosi cha vijana cha Simba ambao ni yeye mwenyewe, Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude pamoja na Said Ndemla.
“Nasema hivyo kwa sababu anajitambua na ni mtu ambaye anapenda mafanikio, kwa hiyo kutokana na kuwa na roho hiyo naamini kabisa kuwa, kasi aliyoanza nayo ndiyo hiyo atakayoendelea nayo kama ambavyo amekuwa akifanya siku zote,” alisema Matola ambaye ni kocha msaidizi wa Taifa Stars.
Sheva hadi sasa ameshafunga mabao mawili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kucheza michezo miwili. Kwa sasa Sheva ndiyo habari ya mjini katika kikosi cha Simba kutokana na uwezo mkubwa ambao amekuwa akiuonyesha uwanjani tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea Lipuli FC.