Lukaku Ampiga Kijembe Ole, eti Conte ni kocha
0
September 23, 2019
MILAN, ITALIA. STRAIKA, Romelu Lukaku ni kama amempiga kijembe Ole Gunnar Solskjaer kiaina baada ya kumsifu kocha wa Inter Milan, Antonio Conte na kusema ndiye anayejua namna bora ya kumtumia.
Lukaku ameungana na Conte huko Inter Milan, baada ya jaribio la kumsajili alipokuwa Chelsea kukwama wakati straika huyo wa Kibelgiji alipoamua kwenda kujiunga na Manchester United iliyokuwa chini ya Jose Mourinho miaka miwili iliyopita.
Kwenye kikosi cha Inter chini ya Conte, Lukaku amekuwa kwenye ubora wake, akifunga kwenye Milan derby wakati timu yake ilipojipigia AC Milan 2-0, huku likiwa bao lake la tatu kwenye Serie A msimu huu.
Akizungumza baada ya mechi, Lukaku alisema: “Nimefurahishwa sana na matokeo haya, na pointi tatu hizo kwenye mechi hii spesho kabisa.
"Sasa, tunafikiria mechi ya Lazio, ambayo bila ni ngumu. Uhusiano wangu na Conte? Jamaa ni bonge la kocha kwa sababu anawasaidia wachezaji kukuza soka lao.
"Kwenye umri wangu wa miaka 26, nilihitaji kocha wa aina hii, mtu anayekuhamasisha kila siku. Ninafuraha kuwa hapa chini yake na kuvaa jezi za Inter.”
Maneno hayo ya Lukaku yanaonekana kama kijembe kwa Solskjaer, ambaye wala hakusita kumzuia asiondoke kwenye timu, akimfungulia mlango wa kutokea Man United akimuuza kwa Pauni 73 milioni na kuamua kubaki na washambuliaji Marcus Rashford na Anthony Martial na kinda Mason Greenwood kwenye kikosi chake cha Old Trafford. Lakini, Lukaku tangu atue Inter amekuwa moto, ameshafunga mabao matatu katika mechi tano.
Tags