Tumeshuhudia idadi kubwa ya klabu zikiwemo maarufu zikipigana vikumbo kuwania saini za nyota wanaotamba Ulaya zikitaka saini zao ili kuimarisha vikosi vyao.
Pia tumeshuhudia mikikimikiki ya mastaa mbalimbali walivyokuwa wakipambana kuzihama klabu zao na kwenda kusaka malisho katika maeneo mengine.
Ingawa ligi bado mbichi, lakini baadhi ya wachezaji wameanza kuonyesha makali yao kwa kufunga mabao katika mechi zao za mwanzoni.
Spoti Mikiki inakuletea majina ya washambuliaji wanane walioanza kwa makeke katika ligi za ndani Ulaya na kuzibeba moja kwa moja klabu zao.
Mbwana Samata
Nahodha huyo wa Tanzania ameanza msimu kwa kasi baada ya kufunga mabao matatu na kuipa KRC Genk ushindi dhidi ya Waasland Beveren.
Pia Samatta alifunga bao dhidi ya Mechelen na Anderlecht hivyo kufanya timu yake kuwa na pointi tisa katika michezo yote na kufikisha mabao matano sawa na Dieumerci Mbokani wa Royal Antwerp.
Teemu Pukki
Pengine kwa michezo michache iliyochezwa hakuna aliyetegemea kuwa angeweza kutokea mchezaji wa aina hii hasa kwa timu kama Norwich City ambayo imepoteza michezo miwili kati ya mitatu ya ligi.
Nyota huyo raia wa Finland amekuwa wa kwanza kufunga mabao matatu ‘hat-trick’ katika msimu mpya England akifanya hivyo dhidi ya Newcastle United. Mshambuliaji huyo alifunga mabao hayo matano dhidi ya Liverpool, Chelsea na Newcastle.
Raheem Sterling
Licha ya kucheza nafasi ya pembeni, mchezaji huyo raia wa England alianza vyema msimu mpya chini ya kocha Guardiola kwa kufunga magoli matano katika mechi tatu za kwanza za ligi hiyo.
Mkali huyo amekuwa na mchango mkubwa sana kwenye kikosi cha timu hiyo kwani uwezo wake, kasi na muunganiko mzuri katika timu hiyo ulimfanya katika mechi tatu za kwanza kulingana Pukki wa Norwich kwa kufunga mabao matano.
Romelu Lukaku
Mshambuliaji huyo aliyemtika Manchester United na kujiunga na Inter Milan ameanza kuonyesha moto baada ya kufunga katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Lecce katika mechi ambayo walishinda mabao 4-0.
Licha ya kufunga bao, Lukaku pia alionyesha kiwango bora katika mchezo huo ukiwa wa kwanza tangu aliposajiliwa kwa kitita cha Pauni73 milioni majira ya kiangazi.
Antoine Griezmann
Kinara huyo wa mabao ametua Barcelona akitokea Atletico Madrid katika usajili ambao ulileta utata baada ya pande zote tatu kuibua mzozo kabla ya kutua Nou Camp kwa Pauni107 milioni.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa, baada ya kuanza kwa kusuasua mechi ya kwanza, alithibitisha ubora wake alipofunga mabao mawili dhidi ya Real Betis katika raundi ya pili ya mechi za La Liga.
Griezmann ameongoza mashambulizi Barcelona baada ya Lionel Messi na Luis Suarez kuwa majeruhi.
Artiz Aduriz
Akiwa ndiye mchezaji mzee zaidi katika Ligi Kuu Hispania, mwenye miaka 38, mshambuliaji huyo raia wa Hispania amezidi kuonyesha bado wamo baada ya kufunga bao dhidi ya Barcelona akitokea benchi benchi.
Aduriz alifunga bao hilo kali la ‘tik-taka’ katika dakika ya 89 na kuipa timu yake ushindi wa 1-0 na kuibuka shujaa wa mchezo huo huku akidhihirisha ubora wake.
Robert Lewandowski
Katika dakika 180 za michezo miwili, mkali huyo mwenye mabao ya kila aina, alifunga matano yakiwemo matatu (hat trick) aliyofunga dhidi ya Schalke 04 katika mechi ya Ligi Kuu Ujerumani.
Mkali huyo aliyewahi kucheza Borussia Dortmund alifunga mabao mawili dhidi ya Hertha Berlin. Nguli huyo anapewa nafasi ya kuingia katika mbio za kuwania kiatucha dhahabu.
Lorenzo Insigne
Kiungo huyo mshambuliaji kutoka Italia ameanza vyema mchezo wake wa kwanza wa ligi hiyo ‘Serie A’ kwa kufunga mabao mawili dhidi ya Fiorentina.
Isigne ni miongoni mwa wachezaji tegemeo na amekuwa akifanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na mingine wanayoshiriki. Mshambuliaji huyo amenza kufungua akaunti ya mabao msimu huu.