BAADA ya kuondoka nchini na kwenda Ubelgiji, Kelvin John 'Mbappe' amesema anaona mwanga kuwa mchezaji mkubwa kwa siku za usoni ambaye atalisaidia Taifa kwenye mashindano mbalimbali.
Mbappe huyo wa Tanzania, aliangwa na wachezaji wanzake wa Ngorongoro Heroes jana Alhamis huku akisafari usiku wa kuamkia leo Ijumaa kupitia nchini Uholanzi kabla ya kuingia Ubelgiji.
“Nilipambana kuzitumia nafasi kadhaa ambazo nilipata za kwenda kufanya majaribio lakini naona sikuandikiwa kuanzia huko ndio maana naenda Ubelgiji ambako nimealikwa.
“Furaha yangu ni kucheza soka Ulaya, nimekuwa nikizungumza na Mbwana Samatta na nina imani kuwa ataendelea kuwa msaada kwangu kama mdogo wake,” alisema wakati akiwa safarini kinda huyo.
Katika barua ya mualiko wake, imeeleza kuwa kuna makubaliano ambayo yanaenda kufanyika kabla ya kinda huyo wa Kitanzania kutambulishwa rasmi kujiunga na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro’.
Kinda huyo ambaye amegharamiwa kila kitu na Genk atafikia M-Hoteli, aliwahi kufanya majaribio na kufuzu chinini Afrika Kusini klabu ya Ajax Cape Town huku akitazamwa na kipa wa zamani wa Manchester United, Edwin van der Sar.
Edwin van der Sar alienda Afrika Kusini kutokana na mahusiano yaliyopo baina ya Ajax ya Uholanzi ambayo alikuwa akiifanyia kazi na timu hiyo yenye maskani yake Cape Town.
Mbappe ataungana na Faissal Boujemaoui wa Morocco ambaye alikuwepo nchini hapa akilitumikia Taifa lake kipindi cha fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 kwenye akademi ya timu hiyo.