Mchungaji maarufu nchini Kenya, Pastor Ng’ang’a ameibua mijadala mizito nchini humo baada ya video za Ibada yake kusambaa mitandao zikimuonesha akiwachapa makofi waumini wake.
Mchungaji huyo wa Kanisa la Neno Evangelism Centre, ameonekana kwenye video hiyo akimuombea kijana mmoja mbele ya madhabahu huku akimchapa makofi kichwani.
Alipomaliza kumchapa makofi kijana huyo, Alihamia kwa waumini wengine na alianza kutembeza kichapo kwa waumini wote bila kueleza sababu ya kufanya hivyo. Bado haijabainika tukio hilo limetokea lini na alikuwa na lengo gani.
Tukio hilo sio la kwanza, Kwani Mchungaji huyo amekuwa akifanya matukio ya ajabu katika maombi yake, Jambo ambalo linawafanya Wakenya wengi waamini kuwa anatafuta kiki kupitia neno la Mungu.
Miezi miwili iliyopita, Pastor Ng’ang’a alionekana kwenye video akimuombea muumini mmoja kwa kumkaba kwenye shingo hadi kuzimia, Huku akikemea kwa kusema anamtoa pepo la umalaya.
Kufuatia matukio hayo, Leo Septemba 17, 2019 Mkurugenzi wa Bodi ya Filamu nchini humo, Dkt. Ezekiel Mutua ametoa onyo kwa viongozi wa Serikali na wa Dini waache kutumia lugha chafu au vitendo vya ajabu pindi wanapokuwa kwenye majukumu yao.
Mutua amesema kuwa Wakenya ni lazima warudi kwenye mstari wa zamani ili kurudisha maadili mema yanayoonekana kuporomoka siku hadi siku.