KIUNGO mkabaji wa Simba, Jonas Mkude amelizua jambo jipya ndani ya kikosi hicho baada ya juzi Jumatano kujiondoa katika kambi ya timu hiyo kwenye Hoteli ya Sea Scape jijini Dar kisha kuingia mitini na kuikacha safari ya kikosi hicho wakati wakielekea mkoani Kagera.
Inadaiwa Mkude alijiondoa muda mchache kabla ya kikosi hicho kuondoka Dar kwenda Kagera ambapo jana Alhamisi walikuwa wanacheza na Kagera Sugar kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani humo.
Kiungo huyo hakuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji 22 licha ya kocha wa Simba kumpigia hesabu ya kuwa miongoni mwa watu ambao angewatumia kwenye mechi hiyo.
Habari za ndani zinaeleza kuwa Mkude aliondoka ndani ya kambi hiyo usiku, siku moja kabla ya safari ambapo wakati msafara mzima wa Simba ukienda Kagera yeye hakuwa miongoni mwao.
“Aliondoka hapa kambini usiku na haikujulikana ameenda wapi. Kocha Patrick Aussems alikuwa ameshamjumuisha kama mmoja wa watu ambao watakuwa kwenye safari hiyo.
“Tangu alipoondoka haijajulikana ameenda wapi kwa sababu akitafutwa hapatikani,” kilisema chanzo hicho.
Alipopatikana kwa njia ya simu Mkude na kuulizwa juu ya suala hilo alikanusha kwa kusema: “Siyo kweli hizo taarifa, mimi nipo.” Alipotakiwa kufafanua zaidi hakujibu chochote.”
Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingiza alisema: “Tunaelekeze nguvu kwenye mchezo wa leo jioni (jana), kikosi kitatoka na utapata taarifa baadaye, hilo suala (la Mkude) halipo kwenye mipango yetu kwa leo.”