Moto wawachoma na kuwaua wanafunzi 23 karibu na mji wa Monrovia Liberia
0
September 18, 2019
Moto umechoma shule ya mnabweni katika eneo moja lililopo viungani mwa mji mkuu wa Liberia Monrovia na kuwaua watoto 23. Moto huo unaaminika kuanza mapema alfajiri wakati wanafunzi hao walipokuwa wakilala katika bweni moja lililoshikana na msikiti.
Polisi wameambia BBC kwamba wanaendelea kusaka miili katika vifusi vya jengo hilo.
Rais George Weah ametuma ujumbe wa Twitter katika rambirambi zake kwa familia za waathiriwa
Msemaji wa Polisi Moses Carter aliambia chombo cha habari cha Reuters kwamba huenda moto huo ulisababishwa na umeme , lakini uchunguzi unaendelea.
Maafisa waliambia AFP kwamba waathiriwa walikuwa kati ya umri wa miaka 10 hadi 20
Mwandishi wa BBC Jonathan Paye-Layleh amesema kwamba ambalensi za shirika la msalaba mwekundu tayari zimechukua miili kutoka eneola tukio na kuna mipango ya kuizika siku ya Jumatano jioni.
Mamia ya watu walikongamana katika shule hiyo kufuatia mkasa huo.
Muhubiri Emmanuel Herbert aliyeshuhudia tukio hilo aliambia BBC aliamka na kusikia sauti ya moto huo na kupiga kamsa ili kutafuta usaidizi.
Nilipotoka nje na kutazama eneo lote lilikuwa jekundu: Nilipotazama dirishani niliuona eneo lote limeshika moto , aliambia BBC.
Lakini alisema kwamba hakuweza kuingia katika jengo hilo kwa kuwa lilikuwa na mlango mmoja pekee ambao ulikuwa umefungwa.