Mtoto Neema Nurdin (8) mkazi wa Kijiji cha Msijute Wilayani Mtwara, aliyedaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha kwa siku 31 na kurejeshwa nyumbani kwao Septemba 18, amemtaja mtu aliyemrudisha kuwa ni mjomba.
Akizungumza leo Septemba 20, 2019 na EATV&EA Radio Digital, Kamishina msaidizi wa jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara Ronald Makona, amesema bado wanaendelea na uchunguzi ili kuweza kumbaini huyo mjomba ni nani kwakuwa Neema alifika nyumbani kwao akiwa peke yake.
''Alitokea tu nyumba ya jirani na kusema kuwa ameletwa na mjomba wake ambaye hakuweza kuonekana, baada ya kuonekana alikuwa ni dhaifu, tulimpeleka hospitali kwa ajili ya kupata matibabu na kupimwa ili kujua kama kuna vitu ambavyo si vya kibinadamu amefanyiwa, majibu ya daktari yanaonesha alikuwa dhaifu kulingana na lishe duni''amesema Makona.
Kupatikana kwa mtoto huyo kumekuja ikiwa ni siku moja tu kupita, tangu Mkuu wa mkoa huo Gelasius Byakanwa kulitaka Jeshi la Polisi, kushirikiana na jamii kuhakikisha mtoto huyo anapatikana, agizo hilo alilitoa Septemba 17 na Septemba 18 mtoto alirejea nyumbani.
Kwa mujibu wa Kamanda Makona mtoto Neema amelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Ligula na kwamba wanategemea akiruhusiwa, watamfanyia mahojiano ili kubaini alikuwa amehifadhiwa wapi.