Mwanamke mmoja kutoka nchini Uingereza aitwaye Kate Cunningham, ameamua kuishangaza jamii kwa uamuzi wake wa kufunga ndoa na mti. Cunningham ni mkazi wa Mjini Merseyside, Uingereza na harusi yake ilifungwa katika moja ya kumbi maarufu nchini humo, Merseyside Park.
Si kwamba hajawaona wanaume, bali ni kwa sababu ya kufanya kampeni za kupinga ujenzi wa barabara, ambao kwa namna yoyote ile mti huo mkubwa na mingine iliyoko katika eneo la Rimrose Valley Park ingelazimika kukatwa.
“Nimekuwa nikiingia mitaani na maelfu ya watu kupinga uharibifu wa miti, lakini sioni hiyo ikiwa na nguvu zaidi kuwaamsha watu,” anasema Cunningham.
Wakazi wa Rimrose Valley Park, hawataki kuona eneo hilo likikatwa miti na kisha ipite barabara kwa kile wanachodai kuwa ni kwa usalama wa afya zao.
“Hii inanigusa moja kwa moja. Mama yangu alifariki kwa pumu na mimi nasumbuliwa na ugonjwa wa mapafu… kuharibu eneo hili na kisha kuweka barabara haiingii akilini na ni hatari wa afya zetu,” anasisitiza.
Si tu kuolewa, wanaharakati wa Mjini Liverpool wamesema Cunningham anataka kwenda mbali zaidi kwa kubadilisha jina lake, ili aitwe aina ya mti huo. Yaani atafahamike kwa jina la Kate Rose ‘Elder’.
“Nataka watu wajikite zaidi katika kampeni ya kuyalinda mazingira ya kijani. Kuna kundi kubwa la watu wasio na uelewa wa kutosha juu ya kinachoendelea,” anaeleza.
Katika picha za siku ya harusi yake hiyo, mwanamke huyo mwenye watoto wawili anaonekana akiwa amevaa gauni la rangi ya kijani, sketi, huku akiwa ameshika maua.
Sherehe hiyo ilishuhudiwa na mamia ya majirani zao, ikinogeshwa zaidi na ‘shoo’ ya mwamuziki mwenye jina kubwa katika eneo hilo, ambaye pia ni mwigizaji, Davy Edge.
Kilichoshangaza zaidi ni kitendo cha mpenzi wake kukubali kushuhudia mwenza wake akifunga ‘pingu za maisha’ na mti huo.
“Mpenzi wangu ananiunga mkono kwa kila ninachoamua,” anasema Cunningham siku moja kabla ya siku ya harusi na kuongeza: “Alinisaidia hata katika maandalizi ya sherehe.”
Wakati huo huo, Cunningham anaongeza kuwa haikuwa rahisi kwake kufunga ndoa na mti huo kwa sababu mtoto wake wa kiume alimwekea ngumu, akionesha kutokubaliana na kile alichotaka kukifanya.
“Mwanzoni mtoto wangu mkubwa aliiona kuwa ni aibu nilipomwambia nitafanya hivyo, lakini kwa sasa amekubali kuja kwenye sherehe. Hiyo ina maana kubwa kwangu,” alisema kabla ya sherehe yake ya kuolewa na mti.
Aidha, anaeleza namna wazazi wake walivyouchukulia uamuzi wa kuolewa na mti, akisema baba yake alikuwa mstari wa mbele kumuunga mkono, akishiriki katika kila hatua ya maandalizi ya sherehe.
Akisimulia ilivyokuwa, hata kufikiria kufanya tukio hilo la aina yake, Cunningham anaeleza: “Lilianza kama wazo tu, kisha tuliona kuwa inawezekana kufanyika. “Nilihamasihwa na wanaharakati wa kike kutoka Mexico, ambao pia waliwahi kufanya kama hivi ili kupinga ukatili dhidi ya miti na uharibifu wa ardhi,” anasema.
Wakati tukio la Cunningham likionekana kuwa habari kubwa kwa sasa, ifahamike kuwa huyo si mwanamke wa kwanza kuamua kufunga ndoa na viumbe visivyo binadamu, iliwahi pia kutokea Julai, mwaka huu ambapo mwanamke aliyefahamika kwa jina la Elizabeth Hoad, aliamua kutangaza kuingia kwenye ndoa na mbwa wake aitwaye Logan baada ya kuchoshwa na wanaume.
Akihojiwa na waandishi wa habari juu ya uamuzi wake huo, Elizabeth anasema kabla ya kumgeukia mbwa wake huyo, alishawahi kutoka kimapenzi na wanaume 221. “Wamenichosha, ni bora niolewe na mbwa wangu,” anasema.
Anasema si yeye tu aliyeamua kufanya hivyo kwani ana marafiki zake 10 waliofanya mbwa kuwa waume zao wa ndoa.
Matukio mawili hayo yanaendana kabisa na lile la mwaka 2015, ambapo Barbarella Buchner, raia wa Uingereza, naye alifanya sherehe kubwa ya kufurahia miaka 10 ya ndoa yake na paka wawili.
Ukiacha hao, yupo mwanamke mwingine Amanda Large Teague, ambaye aliutangazia ulimwengu kuwa ameachana na shetani mwenye umri wa miaka 300, ambaye anasema walikuwa mke na mume. Alichokisema Amanda raia wa Jamhuri ya Ireland ni kwamba aliikimbia ndoa hiyo kwa sababu mumewe huyo alitaka kumuua.
Chanzo Mtanzania digital