Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali imedhamiria kutatua kero za wafanyabiashara ambapo kwa mwaka huu wa fedha imefanya mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kusikiliza changamoto za wafanyabiashara na wawekezaji uliofanyika Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Dkt. Kijaji amesema kuwa moja ya sheria ya kodi iliyofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Kodi ya Mapato."Miongoni mwa sheria zilizofanyiwa mabadiliko mwaka huu wa fedha wa 2019/20 ni pamoja na sheria ya kodi ya mapato ambapo tumepunguza viwango vya kodi kwa wafanyabiashara wadogo," alisema Dkt. Kijaji.
Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa hapo awali wafanyabiashara wenye mauzo ghafi ya kuanzia shilingi 4,000,000 hadi 7,000,000 kwa mwaka walikuwa wanalipa shilingi 150,000 lakini baada ya mabadiliko ya sheria hiyo, kiwango hicho kimepungua hadi kufikia shilingi 100,000 kwa mwaka.
Kwa upande wa wafanyabiashara wenye mauzo ghafi kuanzia shilingi 7,000,000 hadi 11,000,000 walikuwa wanalipa shilingi 318,000 baada ya mabadiliko ya sheria ya kodi ya mapato kiwango hicho kimepunguzwa hadi kufikia 250,000 kwa mwaka
Dkt. Kijaji ameongeza kuwa, kwa wafanyabiashara wenye mauzo ghafi kuanzia shilingi 11,000,000 hadi 14,000,000 walikuwa wanalipa shilingi 546,000 ambapo baada ya mabadiliko ya sheria kiwango hicho kimepungua hadi shilingi 450,000 kwa mwaka.
Vilevile, Naibu Waziri Kijaji amefafanua kuwa, kero nyingine iliyotatuliwa kupitia sheria hiyo ni ile ya wafanyabiashara kuanza kulipa kodi hata kabla ya kuanza kufanya biashara zao ambapo kwa sasa watatakiwa kulipa kodi ndani ya miezi 6 baada ya kuanza biashara.
"Nikisema serikali imedhamiria kutatua kero za wafanyabiashara mjue imedhamiria kweli. Hapo awali, wafanyabiashara wengi walililamikia kitendo cha kuanza kulipa kodi wakiwa ndio wanaanza biashara, lakini mwaka huu wa fedha yamefanyika mabadiliko na sasa wafanyabiashara wapya wataanza kulipa kodi ndani ya miezi 6 wakiwa tayari wamekwishaanza biashara zao," alisisitiza Dkt. Kijaji.
Mkutano huu wa mashauriano kati ya serikali, wawekezaji na wafanyabiashara ni moja ya utekelezaji wa maagizo ya Rais John Pombe Magufuli aliyoyatoa mwezi Juni, 2019 alipokutana na wafanyabiashara Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo aliiagiza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na wizara zote zinazohusika na wafanyabiashara na wawekezaji nchini kwa lengo la kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.