SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema Mbunge Miraji Mtaturu, ni mbunge halali wa Singida Mashariki, kwa mujibu wa sheria baada ya mbunge wa awali, Tundu Lissu, kuvuliwa ubunge kutokana na kukiuka taratibu za kisheria.
Spika amewataka wabunge kuwa na nidhamu na kufuata taratibu za bunge ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa na kuomba udhuru inapotokea wanaumwa au la.
Mapema leo, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam , imetupilia mbali maombi ya Tundu Lissu kupinga uamuzi wa Ndugai kumvua ubunge kwa maelezo kuwa alipaswa kuweka pingamizi dhidi ya uchaguzi na si kuomba mahakama ibatilishe uamuzi wa spika.
Jaji Matupa amesema, hawezi kufanya maamuzi ya kufuta uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa sababu ataingia kwenye mgogoro wa kikatiba na mhimili wa bunge.
Akiendelea kufafanua, Jaji Matupa amesema, endapo maombi hayo ya Lissu yakisikilizwa mpaka mwisho na Lissu akashinda kesi hiyo, Jimbo la Singida Mashariki litalazimika kuwa na wabunge wawili (yaani Tundu Lissu na Miraji Mtaturu) kwa wakati mmoja.