Hatimaye mazishi ya mmoja wa mapacha ANISIA BERNATUS aliyefariki katika hospitali ya taifa muhimbili siku chache baada ya kurejea nchini wakitokea saud Arabia kufanyiwa upasuaji wa kutenganishwa yamefanyika kijijini mabale kata ya mabale wilayani missenyi huku vyombo vya habari vikipongezwa kwa kuibua jambo hilo na kupelekea mapacha hao kupatiwa msaada.
Akitoa salamu za rambi rambi kwa niaba ya serikali,mkuu wa wilaya ya missenyi kanali DENICE MWILA amesema kuwa vyombo vya habari hususani redio za kijamii zilizofika omkajunguti na kuripoti tukio la mapacha hao kuzaliwa,vilisaidia kuuhabarisha umma na kupelekea kupatikana misaada mbali mbali kutoka kwa wahisani na wasamaria wema.
Hata hivyo kanali MWILA ametoa pongezi kwa ubalozi wa Tanzania nchini Saud Arabia pamoja na serikali nchini humo kwa kugharamia safari na upasuaji wa mapacha hao pamoja na hospitali zote zilizoshiriki kuwasaidia.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa watoto kutoka hospitali ya taifa muhimbili dokta ZAITUN BOKHARY amesema kuwa safari pamoja na upasuaji wa mapacha hao umegharimu jumla ya dola za kimarekani elfu 5 za kimarekani zilizotolewa na serikali ya Saud Arabia.
Hata hivyo ameeleza kuwa tatizo lililopelekea pacha ANISIA kupoteza maisha ni kuwa alianza kutapika wakiwa kwenye ndege kutoka Saud Arabia kuja nchini na walipofika nchini walimpeleka moja kwa moja katika hospitali ya taifa muhimbili ambapo alipoteza maisha akiwa katika chumba cha uangalizi maalum.