Mkongwe wa Hip Hop nchini ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mh. Professor Jay ametoa neno kwa wasanii wa Hip Hop Tanzania wanaoshindwa kujiweka kibiashara ili kujiingizia kipato nje ya muziki wanaoufanya.
Akiizungumza na EATV & EA Radio Digital Prof Jay amesema wasanii wengi hawajiongezi kama wasanii wanaoimba na ndio maana inatokea mazingira wanakosa dili mbalimbali ambazo zinawafaidisha waimbaji pekee.
“Mtu anayeimba anapata 'deal' halafu mtu wa Hip Hop hapati na wapo kwenye nchi moja maana yake kuna mmoja anajiongeza na mwingine hajiongezi, kwa sababu hata haya makampuni na mikataba ya kibiashara hauwezi kuvipata kama umekaa nyumbani sebuleni wakuletee lazima uvihangaikie kuvipata, nia kwamba tumekuwa wazembe”, amesema Prof. Jay.
Ameendelea kusema watu wa Hip Hop wanapata tabu kwa kuwa nyuma lakini anaamini wana faida kubwa kwa sababu wanafanya vizuri kwenye 'show' kuliko wanaoimba na hata mitaani wanakubalika.
Aidha amemtaja msanii wa kike Maua Sama ndiye anayestahili kuwa malkia wa Bongo kwa sababu anaijua historia yake tangu anahangaika kutoka kimuziki hadi sasa anavyoelekea kuwa shujaa.