ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, amewatawaka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuhakikisha wanaipa sapoti Yanga kuelekea mechi yao dhidi ya Zesco United, leo.
Yanga watakuwa na kibarua kizito kukipiga na miamba hao wa Zambia ambao tayari wameshawasili jijini Dar es Salaam tangu Jumatano iliyopita, katika mchezo wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Rage amesema suala la uzalendo ni muhimu kwa taifa letu sababu unatia hamasa haswa timu zinapocheza mashindano ya kimataifa. Mwenyekiti huyo wa zamani amefunguka kwa kupingana na Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, ambaye amekuwa akihamasisha mashabiki wa timu yake waende kuishabikia Zesco kuwa si sahihi kufanya hivyo.
“Unajua linapokuja suala la uzalendo sote tunapaswa kuwa wamoja sababu itatusaidia katika mashindano.
“Kwanza naomba ijulikane tu kuwa kama Yanga wakifanya vema kama ilivyokuwa kwa Simba msimu uliopita, tutakuwa na timu nne zitakazoshiriki mashindano kutoka Tanzania.
“Hakuna haja ya kwenda kuwazomea Yanga, sisi tunapaswa kuinyanyua bendera ya taifa letu, pale Taifa hatuna bendera ya Simba wala Yanga,” alisema Rage ambaye amewahi kuwa kiongozi wa TFF enzi za FAT.
Kwa upande mwingine, Rage amewaasa wachezaji wa Yanga kuhakikisha wanajiamini pindi watakapokuwa wanakabiliana na Zesco ili kupata morali ya kupata matokeo.
Amewataka ni vema wakacheza kwa mbinu za kufunguka na kulinda lango lao ili wasiruhusu kufungwa na vilevile wafanye vile wawezavyo waweze kupata bao la mapema ili kujitengenezea mazingira ya kufunga mabao mengine zaidi.
Stori na George Mganga, TUDARCo