Rais Magufuli Atoa Maagizo Mazito Kwa Watendaji wa Kata Nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watendaji Kata nchi nzima, kutembea kifua mbele na  kwa kujiamini kwa kuwa wao ni wawakilishi wake katika ngazi ya kata na hivyo amewataka wasimamie vema miradi ya Serikali ambayo inatekelezwa kwenye maeneo yao.“Cheo cha ofisa mtendaji wa kata siyo kidogo, ninyi ni wawakilishi wangu ngazi ya kata. Tunapozungumza mafanikio ya Serikali ninyi ndiyo wasimamizi wa mwanzo katika mafanikio hayo.

“Kwa hiyo napenda kuwathibitishia ndugu zangu, tembeeni kifua mbele. Wala kamwe asitokee mtu kuwanyanyasa kule mlipo,” amesema Rais Magufuli.


Rais Magufuli ameyasema hayo  Ikulu, jijini Dar es salaam, wakati akizungumza na watendaji hao wa kata, ambapo amewataka licha ya kusimamia miradi ya Serikali, pia kusimamia nidhamu ya watumishi wote wa umma wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, wanaoishi kwenye Kata zao.

"Nyinyi ndiyo wasimamizi wa Watumishi wa Umma kwenye Kata zenu, Mtumishi wa Umma aliyeko kwenye Kata yako, wewe ndiye msimamizi wake, kama kwenye Kata yako yuko RC, Waziri au DC usiogope kumwandikia mapendekezo kama anaenda kinyume na maadili ya kazi zake na ukimuona mkubwa sana nitumie nakala na mimi". amesema Rais Magufuli.Kuhusu majukumu ya watendaji hao, Rais Magufuli amesema maofisa hao wana jukumu la kuhakikisha ulinzi na usalama wa kata zao.

Amewataka pia maofisa hao kuwa makini na utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wageni.

Rais Magufuli amesema kikao hicho ni mwendelezo wa vikao mbalimbali anavyofanya na Watumishi wa Umma, Ikulu, ambapo lengo lake ni kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad