RC Makonda Atangaza Vita Na Watendaji Wanao Mhujumu
0
September 26, 2019
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema katika kipindi cha uongozi wake hajawahi kutoa onyo kwa njia ya barua kwa kiongozi yeyote chini yake ndani ya mkoa huo, lakini sasa ataanza kuwashughulikia kutokana na hujuma anazofanyiwa
Jumapili iliyopita, wakati wa kuwaapisha viongozi aliowateua, akiwamo Mkuu wa Morogoro, Rais Magufuli alionyeshwa kusikitishwa na kusuasua kwa miradi ya maendeleo ilhali mkuu huyo wa mkoa yupo.
Kutokana na madai hayo ya kuhujumiwa, Makonda ametangaza kuwa atawachongea watendaji hao kwenye ngazi za juu za utawala.
Pia amelalamika kuwa amekuwa akitoa maagizo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo lakini badala ya kutekeleza, baadhi ya watendaji hao wamekuwa wakitafuta uhakika kutoka kwa wakuu wa idara.
Makonda aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na wakuu wa wilaya zote tano za mkoa wa Dar es Salaam, wakurugenzi wa manispaa, viongozi wa jiji na watendaji wote katika kikao cha kujadili sababu za kukwama kwa miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Haina maana kama mimi natoa maagizo na nyie viongozi badala ya kuyafuata mnaanza kupitisha vimemo kuuliza kama mtafanyaje ili kutafuta uhakika, ina maana mkuu wa mkoa hana washauri wazuri ndio sababu ya kutofuata maelekezo yake," alisema Makonda.
Alimtaja Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi, ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuwa alikuwa akifuata maelekezo yake bila vikwazo tofauti na viongozi wengine walio chini yake, akiwamo anayeshika nafasi hiyo kwa sasa. Kwa sasa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ni Daniel Chongolo.
"Nilikuwa nikifanya vikao ofisini kwangu na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi na wa Ilala Sophia Mjema. Walikuwa wakifuata ninachowaeleza lakini hawa wengine kila nikiwaambia lazima waanze kupita pita na kuuliza hapa sijamwelewa. Mnapiga majungu yenu, sasa inatosha na mimi nitaanza kuwashughulikia," Makonda alisema.
Alisema viongozi na watendaji wa mkoa huo, wanapaswa kufuata maagizo yake kwa sababu ndiye aliyepewa jukumu la kusimamia mkoa huo.
"Haijalishi kama umenipita umri au nilikukuta serikalini lakini uko chini yangu tu," alisema Makonda na kuongeza kuwa ili kumaliza utata na fitina hizo, naye atakuwa akitoa taarifa za viongozi wasiotimiza wajibu wao kwa viongozi wa juu yake.
Alisema pia kila maagizo atakayokuwa akiwapatia, atakuwa akituma nakala kwa uongozi wa juu ili kuondokana na changamoto ya kuonekana mzembe ilhali anatimiza wajibu wake.
"Tangu nimekuwa mkuu wa mkoa huu, sijawahi kuandika barua kwa viongozi wa juu kumsema kiongozi yeyote, awe mkuu wa wilaya au wakuu wa idara. Lakini sasa nitaanza kuwasema. Nimeshamwambia Katibu Tawala wa Mkoa kila ninapotoa maagizo atoe na nakala kwenda kwa viongozi wa juu," alisema Makonda.
Aidha, aliwataja viongozi wa wilaya ya Kinondoni ambao mradi wa fukwe za Coco umekwama na anapowapa maagizo hawayafuati na kusababisha mkoa kupata sifa mbaya za kukwama kwa miradi.
"Natoa ushauri nyie mnafuata wa kwenu. Nikiuliza mnaitisha vyombo vya habari kusema mnafuata sheria. Mnapindua maagizo yangu na kufuata yenu. Tusishindane, tunapozidiana madaraka kila mtu atimize wajibu wake," alisema.
Tags