Robert Mugabe kuzikwa na familia yake katika uwanja wa mashujaa
0
September 13, 2019
Mwili wa aliyekuwa raisi wa Zimbabwe Robert Mugabe utazikwa kifamilia katika viwanja vya mashujaa, karibu na mji wa Harare, mpwa wake ameiambia BBC.
Leo Mugabe, msemaji wa familia, amesema mazishi hayatafanyika siku ya Jumapili kama ilivyokuwa ikitarajiwa.
Badala yake, mwili wake utapelekwa katika kijiji alichozaliwa Kutama ambapo machifu na wazazi watapata nafasi kufanya shughuli zao za kimila .
Baaadae siku ambayo haijatajwa mwili wa Mugabe aliyefariki juma lililopita akiwa na miaka 95 utazikwa katika uwanja wa mashujaa.
Eneo hilo ndilo serikali ililokuwa inalitarajia kumuhifadhi kiongozi huyo wa zamani.
Na inaonekana kuwa wamefikia muafaka baada ya siku kadhaa za mjadala mkali.
Kumekuwa na mvutano kati ya familia ya Mugabe na wale waliomshinikiza hayati Mugabe kuondoka madarakani kwa mapinduzi mwezi Novemba mwaka 2017.
Awali, Familia ya Robert Mugabe ilisema imeshutushwa kwa kutoshauriwa na serikali kuhusu mipango ya mazishi ya aliyekuwa rais wa Zimbabwe.
Mwili wake unatayarishwa kulazwa ili kupewa heshima za mwisho kitaifa katika uwanja wa soka katika mji mkuu wa Zimbabawe, Harare.
Familia yake na serikali zinatofuatiana kuhusu sehemu atakapozikwa Mugabe.
Familia ya Mugabe inasemekana kuwa na uchungu kwa namna Mugabe alivyotimuliwa na aliyekuwa mshirika wake Mnangagwa miaka miwili iliyopita.
Mugabe alimfuta kazi Mnangagwa mnamo 2017, katika kile ambacho wengi waliamini ni njia ya kumtayarisha Bi Mugabe kumrithi.
Mugabe alikuwa kiongozi wa kwanza wa Zimbabwe baada ya taifa hilo kupata uhuru mnamo 1980. Alishikilia madaraka kwa takriban miongo minne kabla ya kutimuliwa katika mapinduzi mnamo 2017.
Tags