Samatta avaa kitambaa cha unahodha, Genk ikiifunga KV Oostende


Mshambuliaji Mbwana Ally Samatta usiku wa jana alikuwa nahodha wa timu yake, KRC Genk ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya KV Oostende katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.

Mabao ya Genk usiku wa jana yalifungwa na kiungo Mvenezuela Ronald Vargas aliyejifunga dakika ya 18, mshambuliaji Mnigeria Ebere Paul Onuachu dakika ya 44 na kiungo Mnorway, Sander Berge dakika ya 90, wakati bao pekee la lilifungwa na mshambuliaj Mguinea, Idrissa Sylla dakika ya 32.

Ushindi huo katika mchezo wa nane wa msimu, unawafanya KRC Genk, mabingwa watetezi wa ligi hiyo ya Ubelgiji wafikishe pointi 13 sasa wakilingana na AA Gent ambayo hata hivyo imecheza mechi sita na wanaendelea kushika nafasi ya saba.

Samatta mwenye umri wa miaka 26 jana amecheza mechi ya 164 kwenye mashindano yote tangu amejiunga na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa amefunga mabao 68 jumla.

Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 129 na kufunga mabao 52, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja, Europa League mechi 24, mabao 14 na Ligi ya Mabingwa mechi moja, bao moja.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad