Serikali: Hakuna Mgonjwa wa Ebola Tanzania

Wizara ya Afya, Jinsia, wazee na watoto imewatoa hofu wananchi kuhusu ugonjwa wa ebola, ikieleza kuwa imefanya uhakiki na kubaini kuwa hakuna mtu anayeugua ugonjwa huo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Septemba 14, 2019 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa wamefanya uhakiki na matokeo yameonesha kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote wa ebola nchini.

“Ndugu wananchi, Serikali inathibitisha kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa ana ugonjwa huo,” amesema Waziri Mwalimu.

“Hata hivyo, kwakuwa ugonjwa huo umekuwa ukiripotiwa katika nchi jirani, wizara inaendelea kuwakumbusha wananchi kuhusu kuchukua hatua stahiki za kujikinga na ugonjwa huu,” ameongeza.
Waziri Mwalimu ameeleza kuwa wananchi wanapaswa kufahamu dalili za ugonjwa huo ambazo ni homa kali, kuumwa na kichwa, kutapika na kuharisha; viungo vya mwili kuuma, kutokwa na vipele mwilini na kutokwa na damu katika sehemu za matundu za mwili.

Aidha, aliwataka wananchi kutoka maeneo yote nchini kuchukua hatua stahiki kujikinga na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.

“Kwanza tunatoa elimu kwa wananchi kuepuka kugusa damu, mkojo, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye ebola. Pili, tunawataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali na wahudumu wa afya katika maeneo yao pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa ebola au anapofariki mtu mwenye dalili za ugonjwa huo,” alisema Waziri Ummy.

Ugonjwa wa ebola umeripotiwa katika maeneo mbalimbali Afrika ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na hivi karibuni uliripotiwa nchini Uganda.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad