Serikali yaipongeza kampuni ya Route Pro kwa kuwezesha vijana Pikipiki 30


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde (kushoto) akimkabidhi pikipiki, Peter Mushi mkazi wa Makole jijini Dodoma

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Antony Mavunde, ameipongeza kampuni yaya usambazaji bidhaa ya Route Pro kwa ubunifu wake utakaowezesha vijana kupata ajira ambapo imetoa pikipiki 30 kwa vijana katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Arusha, Moshi na Singida ambapo pia itawapatia mafunzo ya biashara.
Mavunde, alitoa pongezi hizo katika hafla ya kampuni ya Route Pro, kukabidhi  pikipiki 10 kwa vijana wa mkoani Dodoma iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini humo.
 “Ukosefu wa ajira kwa vijana ni moja ya changamoto inayolikabili taifa letu, ili kukabiliana na changamoto ambapo Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kushirikiana na wadau wanaoonyesha nia ya kusaidia kubuni mipango endelevu ya kuwezesha ajira kwa vijana, kama  ilivyofanya kampuni ya  Route Pro  kwa kutoa mafunzo ya biashara kwa vijana wetu.  Tutaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kufanikisha suala hili,” alisema Mavunde.


Kampuni ya  Route Pro, itatoa pikipiki 30 kwa vijana sambamba na kuwapatia elimu ya biashara na usambazaji bidhaa, pia itawapatia elimu ya kutumia vifaa vya teknolojia ya kisasa vya kusaidia kuratibu usambazaji na taarifa.  Vijana hao pia itawaunganisha na wadau wake katika biashara na wazalishaji wengine na kushirikiana nao kusambaza bidhaa za wateja katika masoko, mkakati ambao utawanufaisha vijana hao na kampuni kwa kugawana faida itakayopatikana nusu kwa nusu.
Akiongea katika zoezi la  kuwachagua vijana hao, Meneja Uendeshaji wa kampuni ya  Route Pro, Jaja Mbazila, alisema kampuni hiyo imepata walengwa wa kushirikiana nao katika mpango huu, kutokana na rekodi yake ya vijana ambao imewahi kufanya nao kazi katika miradi yake mbalimbali ya usambazaji bidhaa katika siku za nyuma na imewachagua waliokuwa wanafanya kazi kwa bidii na wenye malengo ya kukua kibiashara.

“Tumelenga kuwawezesha vijana wenye bidii ya kazi na kujituma kupata fursa kuwa na biashara zao, tumefanya nao kazi kwa karibu katika miaka iliyopita na wameonyesha kuwa na nia ya kufanya vizuri biashara ya usambazaji,” alisema Mbazila akiongeza kwamba pamoja na kuwapatia pikipiki, Route Pro itawapatia vijana hao kiasi cha shilingi 100,000/- kila mmoja ziwasaidie kuanzia kazi.

Baada ya miezi 24, pikipiki hizo zitakuwa mali yao kwa ajili ya kuwasaidia katika shughuli za usambazaji, ingawa watakaopenda kufanya kazi katika mpango huu wa Route Pro wa kuwawezesha vijana watajiunga tena katika mpango wa miaka miwili na kupatiwa tena tena pikipiki mpya.
Route Pro ni kampuni ya Tanzania yenye uzoefu mkubwa wa biashara ya usambazaji wa bidhaa ambayo   kwa  sasa inazo pikipiki zaidi ya 250 za usambazaji nchini kote na inatumia teknolojia ya kisasa kupata taarifa za mauzo kwa ajili ya kuzifanyia uchambuzi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad