Serikali Yakipa Siku 7 Kiwanda cha Dangote


Lindi. Serikali ya Tanzania imetoa siku saba kwa kiwanda cha kutengeneza saruji cha Dangote kilichopo Msijute, Mtwara kuwasilisha taarifa ya utendaji wake katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kwenda na matakwa ya sheria na taratibu za nchi.

Hayo yameelezwa Na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji, Angellah Kairuki wakati akizungumza na wafanyabiashara mkoani Lindi baada ya kubaini uongozi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na Aliko Dangote kutowasilisha taarifa hizo katika kipindi cha miaka mitatu.

“Nimesikitishwa sana na suala hili la kutopeleka taarifa zenu TIC na mnajua kuwa jambo hili ni la kisheria, kuanzia sasa nawapa wiki moja hakikisheni taarifa hizo zinawasilishwa haraka,” amesema Angellah.

Waziri huyo alieleza hayo akiwa ameambatana na naibu Waziri wa Ardhi, Angela Mabula ambao kwa pamoja walitembelea mgodi wa madini ya uno uliopo kijiji cha Matambalale kusini mwa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Meneja wa kampuni ya Lindi Jumbo inayochimba madini hayo, Paul Shauri amesema mgodi utajengwa kwa miezi tisa na wanatarajia kuwekeza zaidi ya dola milioni 30 za Marekani,  sawa na Sh69 bilioni.

Akifafanua zaidi Angela ameziagiza Halmashauri zote kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi katika vijiji vyenye maeneo ya uwekezaji.

“Hakuna sababu ya mwekezaji kuanza kuhangaika na mambo madogo kama hayo ambayo yanampotezea wakati,  ni lazima halmashauri zijipange ili kumwekea mwekezaji mazingira mazuri avutiwe kuwekeza” amesema Angela.

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa ameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara za wilaya hiyo ili kuchochea mazingira ya uwekezaji wa kampuni zilizoonyesha dhamira ya kuwekeza.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad