Stella: Dereva wa malori ya masafa marefu aliyetekwa DRC
0
September 01, 2019
“Niliwahi kutekwa na waasi nikiwa njiani napeleka mafuta Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ilikuwa siku ngumu kwangu, lakini haikunikatisha tamaa wala kunirudisha nyuma katika kazi yangu ya udereva wa magari makubwa,” anaanza kusimulia Stella Aladin ambaye ni miongoni mwa wanawake wachache wanaoendesha magari makubwa ya safari ndefu.
Stella ambaye kwa mwonekano ni mwembamba mrefu wa wastani, ni miongoni mwa madereva watatu wa kike waanzilishi wa kuendesha magari makubwa ya safari ndefu.
Ameifanya kazi hiyo kwa miaka 22 na kwa sasa ameajiriwa kwenye kampuni ya ZH Poppe inayomilikiwa na mwanachama na mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hanspoppe, kama dereva wa magari ya matanki ya mafuta.
Mbali na kuendesha magari makubwa ya matanki, Stella amewahi pia kuendesha mabasi ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani kwa miaka sita mfululizo.
“Nilianza kupenda kuendesha magari makubwa nikiwa shule ya msingi,” anasema Stella japo hakutaka kueleza ni shule ipi na wapi akifafanua kwamba wakati wa utoto wake alipenda kuendesha magari ya ‘matoi’ makubwa yenye matela kama wafanyavyo watoto wa kiume.
Anasema akiwa nyumbani alijifunza kuendesha gari ndogo ya kukatia majani, aliyofundishwa na kaka yake, alipomaliza darasa la saba alikwenda kusomea udereva na alipohitimu gari ya kwanza kuendesha ilikuwa Fiat.
“Niliendesha kwa muda Fiat nikarudi shuleni kuongeza ujuzi zaidi kwenye fani ya udereva, nilipohitimu niliajiriwa kwenye kampuni ya mabasi, ilikuwa ni changamoto ya woga, lakini leseni yangu iliniruhusu kwa kuwa ilikuwa kazi ya ndoto yangu niliifanya, ” anasema.
Anasema jamii na hata abiria aliokuwa akiwasafirisha walikuwa wakimshangaa, alipowafikisha salama walikuwa wanampongeza na baadhi yao wakimpa fedha kama shukrani.
Anasema wakati anaanza kazi hiyo, madereva wa kike nchini waliokuwa wakiendesha magari makubwa aliokuwa akiwafahamu walikuwa watatu ambao ni yeye (Stella) mwingine alimtaja kwa jina la Halima na Jane ambaye kwa sasa ni marehemu.
Anasema kwa sasa madereva wa kike wanaoendesha magari makubwa ya safari ndefu anaowafahamu wanafika 20 na wanajuana.
Tags