Kila siku huwa najifunza sana kuhusu fedha na kuhusu tabia za watu kuhusu fedha. Pia nimekuwa nakazana sana kujifunza kuhusu fedha katika miaka mingi iliyopita. Nimekuwa najifunza kuhusu historia ya fedha, historia ya matajiri mbalimbali waliopata kuwepo kwenye uso huu wa dunia. Na muhimu zaidi nimekuwa najifunza kupitia tabia za wengine kuhusu fedha, kwa kuanza na wale watu ambao ni wa karibu sana kwangu. Nimekuwa naona mengi sana kuhusu fedha na tabia za watu. Lakini ipo tabia moja, ambayo kwa kila mtu ambaye amedumu kwenye umasikini kwa muda mrefu, anayo. Watu hawa wanakuwa waaminifu sana kwa tabia hiyo na hivyo kushindwa kabisa kuondoka kwenye umasikini.
Leo kupitia makala hii nitakueleza kuhusu tabia hii, na kuichambua kwa undani halafu nitamalizia kwa kukushauri namna gani ya kuondokana na tabia hii. Nina imani iwapo tutakwenda pamoja hapa, na ukachukua hatua kwa kile utakachojifunza, miaka kumi ijayo, NDIYO NIMESEMA 10, hutakuwa hapo ulipo sasa. Na kama ulifungua hapa kusoma ukijua nakupa mbinu ya kesho kuamka ukiwa tajiri, umepotea njia, nakusihi usiendelee kusoma, maana utakachokutana nacho, hakitakupendeza.
Mwisho kabisa, siyo mwisho wa makala, bali mwisho wa utangulizi na kabla sijaingia kwenye tabia hiyo inayokuzuia usitajirike, niseme wazi kwamba mimi na umasikini hatuwezi kukaa sehemu moja. Kwa akili zangu timamu, niliukana umasikini na kujiambia nitafanya lolote niwezalo, ambalo siyo kinyume na sheria, hata kama itakuwa kukesha usiku na mchana, kuhakikisha naondokana na umasikini kabisa kwenye maisha yangu. Nilijiahidi sitauonea umasikini huruma kabisa, na ninaamini hakuna ufahari wowote kwenye umasikini, japo bado kwenye jamii zetu mtu masikini ndiyo anaonekana ana haki zaidi kuliko tajiri.
Hicho ndiyo nataka na wewe rafiki yangu ukiri leo kwenye maisha yako, na uamke kupambana ili umasikini ukukimbie wenyewe. Lakini lazima kwanza uepuke tabia hii moja ambayo bila kuondokana nayo, mipango yako yote itakuwa ya kujifurahisha tu.
Tabia moja ambayo itakufanya uendelee kuwa masikini ni TABIA YA KUTUMIA KIPATO CHAKO CHOTE.
Rahisi eh! Hukutegemea kama nitakuambia kitu rahisi kama hicho, ambacho tayari unakijua, kila siku umekuwa unajifunza, weka akiba, jilipe mwenyewe kwanza na maneno mengine ambayo huenda unasema ni yale yale. Sawa, lakini kabla hujasema ni rahisi na kuacha kusoma ili uendelee na yako, naomba nikuulize swali moja, pamoja na kujua je unatekeleza?
Unajua kwamba unapaswa kujilipa wewe mwenyewe kwanza, je unajilipa? Unajua unapaswa kuwa na akiba, je una akiba? Najua hujilipi mwenyewe, kwa sehemu kubwa, au hata kama unafanya, siyo nyakati zote. Sasa endelea kusoma hapa, kwa sababu kuna kitu kinakuzuia, ambacho leo tunakwenda kukifunua wazi wazi na kisiendelee kukuzuia.
Tuanzie kwenye historia, maisha ambayo mababu wa mababu zetu waliyaishi. Hapa ndipo pazuri sana ambapo tumebeba tabia hizi zinazotufanya tuwe masikini leo.
Njema ni siku zilizopita, ambapo jamii ilikuwa na wakulima na wafugaji. Ardhi ilikuwa tele na ya kutosha, na chochote ambacho watu walitaka walikipata. Hakukuwa na ajira rasmi wala biashara kubwa, mbadilishano wa thamani ulikuwa rahisi na maisha yalikuwa yanaenda. Ni katika nyakati hizi, ambapo wakulima walilima na kuwa na uhakika wa kuvuna. Na hivyo kabla mavuno mapya hayajavunwa, yale ya zamani yalitumiwa yote, na kama bado yalibaki basi yaliharibiwa kabisa. Watu walianza mwaka mpya wa msimu kwa mazao mapya. Hii ni tabia ya asili kabisa katika jamii zetu nyingi, mababu wa mababu zetu waliishi maisha haya, ambayo walirithi kwa mababu wa mababu zao.
Karibu kwenye dunia ya sasa, ambayo hakuna jambo lolote ambalo watu wanaweza kuwa na uhakika nalo kwa silimia 100. Hakuna kinachoweza kutegemewa tena moja kwa moja, lakini bado ile tabia ya kutegemea kitu moja kwa moja ipo ndani yetu. Na ndiyo maana watu wanapopata kazi, au kuanza biashara, unaanza kuona maisha yao yanabadilika na kuwa tegemezi moja kwa moja kwenye kitu kile wanachofanya.
Hii ndiyo tabia ambayo imekuwa inawafanya wengi waone siyo shida kutumia kila kipato wanachopata. Hata hivyo mshahara si upo mwezi ujao, hakuna shida. Au kama biashara bado ipo, basi kipato bado kipo. Nimekumbuka zamani mtaani kwetu palikuwa na watu ambao wanafanya kazi ya kuongoza watalii kupanda mlima Kilimanjaro. Sasa walikua wakirudi kutoka mlimani, walikuwa na fedha sana, walikunywa na kuwanunulia wengine pombe watakavyo. Na walipolewa, waliwauliza watu, hebu toka nje na chungulia kama mlima upo, wakiambiwa upo wanaendelea kuagiza pombe. Mlima upo, fedha zitaendelea kuwepo.
Nafikiri unaona namna gani hii tabia ipo ndani yetu kabisa, yaani imeweka mizizi kabisa.
Tunapenda kuamini kwamba kitu kitaendelea kuwa kama kilivyo. Lakini huo siyo uhalisia, mambo yanabadilika na hakuna chochote ambacho tunaweza kuwa na uhakika nacho. Na mbaya zaidi, utegemezi huu ndiyo umekua unaleta umasikini mkubwa.
Hivyo rafiki yangu, tabia hii ya kuwa na utegemezi mkubwa kwenye jambo lolote, na kutumia kipato chote ambacho unaingiza, bila kuweka pembeni hata senti moja, ni njia ya uhakika ya kuendelea kuwa masikini.
Uchukue hatua gani ili kuondokana na tabia hii?
Kwanza kabisa, ondokana na tabia ya kuwa tegemezi kwenye jambo lolote lile kwenye maisha yako. Hata kama upo kwenye ajira, usijidanganye kwamba itaendelea kuwa hivyo ilivyo. Kama upo kwenye biashara, ndiyo kabisa hupaswi kujichia na kuona umeshashinda, hata kama una wateja wengi mpaka wengine unashindwa kuwahudumia. Jua mara zote kwamba mambo yanabadilika na wakati wowote unaweza usiwe hapo ulipo sasa.
Kwa kufikiri hivyo, utahitaji kuwa na maandalizi mapema, utahitaji kujipanga ili lolote linapotokea, uwe kwenye wakati mzuri wa kuchukua hatua, na hapo utaacha kujiachia na kutumia kama vile hakuna kesho, au kwa kujiaminisha kesho itakuwa kama leo tu.
Kingine muhimu zaidi cha kukuondoa kwenye umasikini, ni kuhakikisha unajilipa wewe mwenyewe kwanza, kwa kuweka pembeni kila sehemu ya kipato chako. Na nisisitize vizuri, hii siyo akiba unayoweka, bali fedha unayojilipa, halafu unaiwekeza ili baadaye iweze kukuzalishia zaidi na zaidi hata kama wewe hufanyi tena kazi.
Hii dhana ya kujilipa wewe mwenyewe kwanza itakuletea uhuru mkubwa sana kwenye maisha yako ukiweza kuiishi. Na unachofanya ni kwa kila kipato unachoingiza, unatenga sehemu ya kumi ya kipato hicho na kuweka pembeni. Kama unapata elfu kumi, unaweka pembeni elfu moja, kama umepata laki, unaweka pembeni elfu kumi, kama umepata milioni unaweka pembeni laki, na kuendelea hivyo. Sasa swali huja, fedha hiyo unaipeleka wapi? Na jibu ni moja tu, unaiwekeza, kwenye maeneo ambayo yataulipa zaidi siku za baadaye. Yapo maeneo tofauti unayoweza kuwekeza, kwenye ardhi na majengo, kwenye soko la hisa, kununua vipande, kuanzisha biashara na kadhalika.
Muhimu sana kwako kwa kuanza, ni kujilipa, kiasi kidogo kidogo na kuwekeza. Ukifanya hivi kuanzia leo, hata ukaanza kwa shilingi elfu moja au elfu tano, miaka 10 ijayo hutakuwa hapo ulipo sasa rafiki yangu. Niamini kwenye hilo na anza kuchukua hatua.