SHIRIKISHO la Soka Tanzania ‘TFF’ limetoa ufafanuzi wa madai ya aliyekuwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Emmanuel Amunike kutinga katika Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa) ikidaiwa anadai fedha zake kwa TFF.
TFF iliachana na Amunike hivi karibuni kufuatia Taifa Stars kufanya vibaya kwenye michuano ya Kombe la Afrika
‘Afcon’ iliyofanyika huko nchini Misri. Juzi, mitandao mbalimbali ya michezo Bongo iliripoti kuwa, Amunike amepeleka malalamiko Fifa akidai malipo yake kwa TFF kutokana na kutommalizia baada ya kuvunja mkataba.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau amefunguka kuwa, TFF haijapata barua yoyote kutoka Fifa juu ya malalamiko ya Amunike kudai malipo yake hadi sasa kwa kuwa wanafanya kazi kwa
ukaribu na kudai kuwa wao kama TFF tayari wameshamlipa kocha huyo kwa asilimia kubwa ya deni lake na iliyobakia ni kidogo.
“Tumekatisha mkataba na kocha wetu Amunike kwa makubaliano maalumu, awali wakati tumeingia mkataba tulikubaliana iwapo tutavunja naye mkataba tutamlipa mshahara wa mwezi mmoja na ndivyo ilivyotokea ambapo jumla alikuwa akitudai fedha ya mkataba wa miezi miezi tatu ambayo tayari tumeshammalizia.
“Fedha anayotudai kocha ni ile ya kusaini mkataba na bonasi ya kuipeleka Stars Afcon ambayo pia tumemuahidi kummalizia na imebakia kidogo sio nyingi. Hata huyo mwalimu nimekuwa nikiwasiliana naye vyema, Jumapili iliyopita alinitumia ujumbe wa kutupongeza kuingia hatua ya makundi ya Afcon, hivyo kama jambo hilo lipo basi angenieleza hata yeye.
“Mkataba ambao tuliingia na kocha safari hii sio kama ile ya nyuma ambayo ilikuwa tatizo
katika kuivunja kutokana na kutakiwa kulipa fedha nyingi kama vile ilivyokuwa kwa kocha Kim Poulsen ambaye alikuwa mkurugenzi wa ufundi alikuwa akidai fedha nyingi.
“Aidha tumepanga hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu tuwe tayari tumeshamlipa aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa, Boniface Mkwasa ambaye naye anadai TFF,” alimaliza Kidau. Waandishi: Khadija Mngwai, Marco Mzumbe na Abdulghafal Ally
TFF: Amunike anatudai lakini, Tumemlipa Asilimia Kubwa
0
September 14, 2019
Tags