Tundu Lissu Akumbuka Miaka Miwili ya Kushambuliwa kwa Risasi
0
September 08, 2019
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amekumbuka miaka miwili tangu ashambuliwe kwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani kwake jijini Dodoma.
Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma nchini Tanzania Septemba 7, 2017 akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge na jana amefikisha miaka miwili akiwa ughaibuni.
Baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kisha usiku wa siku hiyo hiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya hadi Januari 6, 2018 alipopelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambako bado yuko huko mpaka sasa.
Jana mwanasheria mkuu huyo wa Chadema ameandika andiko lenye kichwa cha habari ‘miaka miwili ya mateso, matumaini’, akieleza mambo mbalimbali aliyopitia katika kipindi hicho, kuwashukuru watu wa kada mbalimbali waliomsaidia.
“Kwenye maegesho ya magari nje ya nyumbani kwangu, watu wawili wenye bunduki za kivita waliruka ghafla kutoka kwenye gari iliyokuwa inatufuata kwa nyuma na kuanza kunishambulia kwa risasi nyingi. Kati ya risasi zaidi ya 30 zilizoipiga gari, 16 zilinipiga katika sehemu mbali mbali za mwili wangu. Nilijeruhiwa vibaya,”amesema Lissu.
Anasema pamoja na kuwa ilikuwa mchana katika mji wa kawaida wa Dodoma, na katikati ya vikao vya Bunge ambapo ulinzi huwa mkali, washambuliaji hao walikimbia na kutokomea kusikojulikana.
“Leo hii, miaka miwili baadae, Serikali yetu bado inawaita washambuliaji hao 'watu wasiojulikana.' Hadi sasa, Jeshi la Polisi linadai halina 'taarifa za kiintelijensia' au hata tetesi za waliohusika kwenye kitendo hiki cha kijinai. Hakuna anayeshukiwa.”
“Hakuna aliyekamatwa na kwa hiyo hakuna aliyewajibishwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania,” amesema Lissu.
Hata hivyo anasema baada ya matibabu ya miaka miwili, kwanza katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, na tangu Januari ya mwaka jana katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg, nchini Ubelgiji, sasa anaweza kutangaza hadharani kwamba kwa kiasi kikubwa amepona.
“Nimeacha kutumia magongo tangu Juni 29, 2019 na pia sindano na dawa zote nilizokuwa natumia tangu tarehe 30 Julai.”
“Na kufuatia vipimo nilivyofanyiwa Agosti 20, 2019 madaktari bingwa ambao wamenitibu tangu Januari mwaka jana wamenijulisha kwamba mifupa iliyovunjwa vunjwa na risasi za Septemba 7, 2017 imeunga na kupona vizuri,” amesema Lissu.
Akielezea kuhusu afya yake hivi sasa Lissu amesema vipimo vya damu vinaonyesha kwamba sasa damu yake haina bacteria.
“Kilichobaki ni marekebisho ya viatu maalum nilivyotengenezwa kwa ajili ya kusawazisha mguu wa kulia ambao umekuwa mfupi kuliko mwingine kutokana na majeraha makubwa ya risasi.”
“Baada viatu hivyo kukamilika, nitafanyiwa vipimo vya mwisho Oktoba Mosi na 8, 2019 nitakutana na madaktari wangu ili kupatiwa maelekezo ya mwisho kabla ya safari yangu ya kurudi nyumbani (Tanzania),” amesema Lissu.
Tags