Unaambiwa Harmonize Afanikiwa Kuizima VITA ya Diamond na Ali Kiba....


BADO hali si shwari ndani ya lebo kubwa ya muziki barani Afrika ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ tangu kuondoka kwa mmoja wa memba wake, Rajab Abdul ‘Harmonize’ ambaye sasa amesababisha vita mpya.

HARMONIZE AMALIZA VITA

Awali, kabla ya kukua kimuziki kwa Harmonize au Harmo, ilifahamika kuwa mshindani mkubwa wa Diamond au Mondi alikuwa ni mwanamuziki Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’. Taarifa ikufikie kuwa, mambo yamekorogeka kwani Harmonize anatajwa kumaliza vita ya Mondi na Kiba. Wakati Mondi akimiliki Lebo ya WCB, Kiba anamiliki Lebo ya Kings Music huku Harmonize akiwa ameanzisha ya kwake ya Konde Gang.

HARMO MECHI YA STARS

Kiini cha habari hii ni shoo aliyoangusha Harmonize ndani ya Uwanja Mkuu wa Taifa (maarufu kama Uwanja wa Mkapa) mara baada ya mechi ya Taifa Stars na Burundi ambapo Stars waliibuka washindi kwa matuta 3-0.

Katika shoo hiyo ambayo uwanja ulikuwa umetapika, Harmonize aliangusha shoo ya kihistoria kwa kupiga ngoma zake tatu za Kwangwaru, Kainama na Never Give Up.

MJADALA MZITO

Mara baada ya mechi na shoo hiyo, gazeti hili lilizungumza na mashabiki wa soka ambao walitoa ya moyoni;“Huyu jamaa (Harmonize) amemaliza kabisa ubishi wa Diamond na Kiba na sasa vita ni kati yake (Harmonize) na huyo bosi wake aliyemtoa,” alisema Yusto Kema, Mkazi wa Kigogo, Dar. “Mimi ni mfuatiliaji mzuri wa Muziki wa Bongo Fleva na ni shabiki wa Diamond, lakini acha niseme ukweli, baada ya Harmonize kuondoka Wasafi, ndiye mshindani mpya wa Mondi na siyo Kiba tena.

“Najua ubora wa Diamond, Kiba na Harmonize, nisiwe mnafiki, huyu dogo (Harmonize) amemaliza kabisa ubishi wa Mondi na Kiba nani zaidi. “Nasema hivyo kwa sababu vita mpya kwa sasa ni kati ya Diamond na Harmonize…Konde Boy mwenyewe.

“Iwe ameondoka kwa amani au kwa ugomvi, lakini tunajua kwamba jambo hili haliwezi kumfurahisha Diamond hivyo tutarajie vita nyingine mpya kabisa kwenye Bongo Fleva.

“Hakuna anayeweza kupinga uwezo wa Kiba wa kuimba na kutunga, lakini ukweli ni kwamba katika siku za hivi karibuni amezimwa na vuguvugu kubwa la hawa jamaa wawili wa Wasafi (Diamond na Harmonize).

“Si kwamba Kiba ameshuka kiwango, hapana! Lakini sasa ushindani umehama, hauko upande wake na hata ukiingia kwenye mitandao ya kijamii, utaona habari kubwa ni Harmonize na Diamond.

“Leo hii Kiba akiachia ngoma na Harmonize akaachia, unaweza kuona namna ambavyo Harmonize atapata viewers (watazamaji) wengi kwenye YouTube ukilinganisha na Kiba kwa sababu ndiye anayefuatiliwa zaidi kwa sasa. “Kwa mantiki hiyo utagundua kuwa Kiba ana kibarua kizito cha kukabiliana na Konde Gang na kumwacha mpinzani wake wa takriban miaka kumi iliyopita.

“Kwa mantiki hiyo basi Kiba analazimika kuachia ngazi kwenye ushindani wake na Diamond na kumpisha Harmonize au kama akitaka kukomaa, basi aifanyie marekebisho makubwa lebo yake ya Kings Music ili asitupwe mbali na upepo wa kisulisuli wa Harmonize,” alimalizia Inocent James, Mkazi wa Mbezi-Beach jijini Dar.

MJADALA KAMA WOTE

Kwenye mitandao ya kijamii baada ya ushindi wa mechi ya Stars, shangwe ziliunganishwa na shoo ya Harmonize ambapo kila mtu alikuwa akionesha kumkubali jamaa huyo ambaye kimataifa ameshafanya shoo na wasanii wengi kuliko Kiba.

ISHARA NYINGI

Ishara nyingi za Harmonize kuanza kushindana na Diamond zilianza kama miezi miwili ambapo Mondi alikuwa ameachia wimbo wake mpya akiwa na mwanamuziki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Fally Ipupa. Ndani ya wimbo huo, Diamond anasikika akiimba; “Penzi lilimfanya Harmonize amfukuzishe kazi Mwarabu.”

Ambapo Harmonize alijitokeza hadharani na kumjibu Mondi; “Ndiyo unataka ijulikane kwamba demu wangu alikuwa ana…(neno lisilo na maadili) na Mwarabu?” Kuanzia hapo upepo haukuwa mzuri hadi Harmonize alipoondoka Wasafi.

Lakini maelezo mengine yanasema kuwa tofauti kati ya Mondi na Harmonize zilijidhihirisha zaidi baada Harmo kufika kwenye shoo ya Tamasha la Wasafi jijini Mwanza, usiku akiwa na usafiri wake wa Toyota Coaster iliyokuwa na Nembo za Konde Gang.

Maneno kutoka kwa waja huwa hayakosekani, kuna madai kuwa Harmonize ana usimamizi mpya wa mtu anayetajwa kwa jina la Jembe ni Jembe ambaye naye ana uzoefu na burudani za Bongo.

Baadaye imefahamika kuwa Harmonize ameanzisha himaya yake akiwa na ofisi kubwa ya nyumba nzima maeneo ya Sinza- Kijiweni ambapo ndani yake kuna studio ya kurekodi muziki na timu yake imejikita hapo.

MENEJA WA ZAMANI

Mmoja wa mameneja wa zamani wa Harmonize, Joel Vincent maarufu kwa jina la Mr Puaz anatoa maoni yake juu ya ushindani mpya wa Harmonize na Diamond; “Nadhani hajatoka Wasafi ili kushindana na Diamond, bali anataka mapato mazuri zaidi ya aliyokuwa anayapata. “Hata mtoto mdogo akishakua na kuona kwamba sasa anafaa kuwa na familia yake ataondoka nyumbani kwa wazazi wake na kwenda kujitegemea.”

“Kama ataweza kusimamia vizuri mawasiliano yake na uongozi bila shaka atakua mwanamuziki mkubwa, siyo tu Afrika bali pia duniani. “Natumaini amejifunza mengi kutoka kwa Diamond hivyo basi hatafanya makosa aliyoyaona katika kipindi chake chote na Wasafi,” aliongezea.

ALIKOTOKA HARMONIZE

Harmonize alizaliwa huko Mtwara katika Kijiji cha Chitoholi. Alisoma katika shule ya Sekondari ya Mkundi iliyopo mjini Mtwara. Baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari, Harmonize alielekea jijini Dar ambako huko alijipatia riziki yake ya kila siku.

Mwanzoni mwanzoni alibeba maji ili kupata tonge la chakula, pia alikuwa akiuza kahawa kwa wafanyabiashara wengine na wakazi wa Kariakoo jijini Dar kabla ya sauti yake kutambulika mitaani kisha baadaye kuchukuliwa na Wasafi.

Harmonize alianza kujihusisha na muziki mnamo mwaka 2011 ambapo alitoa nyimbo mbalimbali, lakini hazikuweza kupata umaarufu mkubwa hadi pale ambapo alikutana na Diamond mnamo mwaka 2015 ndani ya Ukumbi wa Dar Live na kuanza kufanya muziki pamoja. Baadhi ya nyimbo zake kali ni pamoja na Aiyola, Bado, Matatizo, Happy Birthday, Niambie, Atarudi, Kwangwaru na nyingine nyingi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad