UPDATE: Mawakili wapinga ndege ya Air Tanzania kuzuiwa Afrika Kusini
0
September 02, 2019
Dar es Salaam. Jopo ya wanasheria waliopelekwa na Tanzania kupinga amri ya kushikiliwa kwa ndege ya Air Tanzania wameiambia mahakama ya Gauteng, Afrika Kusini kwamba amri ya kushikiliwa ndege hiyo ilitolewa kimakosa.
“Tumeonyesha kwamba amri ya kuishikilia ndege ya Air Tanzania aina ya airbus A220-300 ilitolewa kimakosa dhidi ya Serikali, kwa hiyo tumetaka iondolewe,” wakili Ngaukaitobi aliiambia mahakama.
Wakili Roger Wakefied anayemwakilisha mkulima Hermanus Steyn amesisitiza kuwa kuna kesi ya msingi ya kujibu na ameitaka mahakama hiyo kuangalia vigezo vya madai hayo na kuvitendea haki.
Kwa mujibu wa Wakefield hatua ya kwanza ya vigezo vya kesi hiyo vimeshathibitishwa.
Ndege hiyo ilishikiliwa Agosti 23, 2019 nchini humo kutokana na mvutano wa kisheria uliodumu kwa miongo kadhaa kati ya Serikali ya Tanzania na mkulima Hermanus Steyn.
Mali za Steyn ikiwemo kampuni ya mbegu ya Rift Valley Seed Company Limited na mali nyinginezo zilitaifishwa na Serikali ya Tanzania Januari 1982. Amekuwa akiidai Serikali Sh373 milioni.
Hata hivyo, Julai 9, 2010 Jaji mstaafu Josephat Mackanja wa mahakama kuu alimpa Steyn tuzo ya Dola za Kimarekani 36,375,672.81.
Kuna ushahidi kuwa baada ya kutolewa kwa tuzo na Mahakama hiyo kulikuwa na makubaliano kati ya pande mbili yaliyoishusha hadi kufikia Dola 30 milioni na Serikali ya Tanzania ililipa kiasi kikubwa cha deni hilo kupunguza madai hayo.
Akizungumza na gazeti la Daily News, Wakili mkuu wa Serikali, Ally Possi amesema timu ya mawakili wanane kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali watapambana kwenye kesi hiyo iliyotajwa Agosti 21, 2019 ambayo hati ya dharura iliwekwa na kampuni ya mawakili ya Werksman’s Attorneys ikitaka ndege yoyote ya ATCL ili kufanikisha malipo ya tuzo hiyo.
Mwananchi
Tags