Waagizwa Kufuatilia Mtoto Aliyekatwa Mkono Mwananyamala

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee wa Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amemuagiza Msajili wa Baraza la Madaktari la Tanganyika kushirikiana na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania kufuatilia mtoto aliyekatwa mkono baada ya kuhamishiwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala.

Dkt. Ndugulile ametoa maagizo hayo wakati akizindua bodi ya nane ya maabara binafsi za afya kwenye ukumbi wa Veta jijini hapa.

“Nilitegemea baraza la madaktari muwe mmeanza uchunguzi, kwahiyo nakupa maagizo kesi hiyo muanze kufuatilia na kama itathibitika ni uzembe waliohusika wachukuliwe hatua, ndani ya wiki mbili mtuletee majibu ili mimi na Mhe. Waziri tujue tunachukua hatua gani.

Dkt. Ndugulile amesema kwenye mabaraza bado kuna changamoto ya baadhi ya mashauri kuchukuliwa hatua hivyo kama mabaraza ya kitaakluma ni vyema kuangalia ufanisi wa majukumu yao na kuchukulia hatua pale taaluma inapokosewa na waliokosea wachukuliwe hatua.

Dkt. Ndugulile ameitaka bodi hiyo kusimamia usajili wa maabara zote nchini kwani hivi sasa imetokea uanzishwaji wa maabara kiholela zinazotoa huduma kwa wananchi bila ya kusajiliwa hivyo kufanya ukaguzi ili kubaini maabara hizo na kuzichukulia hatua.

“Naomba sheria ifuate mkondo wake ili kubaini wale wote walioanzisha huduma za maabara bila kufuata sheria na taratibu za usajili, tushirikiane kuhakikisha kuwa hakuna taasisi au mtu atakayefungua au kutoa huduma za maabara bila kusajiliwa”. Amesisitiza Dkt. Ndugulile.

Aidha, Naibu Waziri huyo amesema baraza hilo ni chombo muhimu na ndio moyo wa sekta ya afya kwani maabara inatoa muelekeo wa mgonjwa kwa kuthibitisha tatizo, hivyo inahitajika maboresho katika utoaji huduma za maabara.

“Sasa hivi huduma hizi zimekua ni biashara kwani asiliamia 70 ya homa wala sio Malaria ni virusi watu wanakunywa dawa sana pasipo kuzingatia misingi kwani maabara hizi zinatumika kama sehemu ya matibabu na hata upasuaji, mtu anaenda maabara anakaa dakika kumi na tano anaambiwa ana UTI wakati mwingine anaambiwa ana malaria plasi plasi hii maana yake ni nini hili linahitaji ufuatiliaji”. Alisema Dkt. Ndugulile.

Hata hivyo aliitaka bodi hiyo mpya kusimamia ubora wa huduma za maabara ili kuinufaisha jamii na kuhakikisha huduma za afya katika jamii zinaboreshwa kukidhi viwango vitavyotarajiwa na hivyo kuboresha afya na maisha ya watanzania.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la maabara binafsi Prof. Said Abood aliahidi kutekeleza maagizo yote waliyopewa na Naibu waziri ikiwemo ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini maabara bubu na ambazo hazijasajiliwa pamoja na kuhakikisha maabara zinatoa huduma zinazostahili ili kuweza kumsaidia daktari kumpatia mwananchi huduma stahili

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad