Waitara: Wakuu wa Mikoa na Wilaya Hawana Mamlaka Kusimania Uchaguzi.
0
September 06, 2019
Na .Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), MWITA WAITARA amesema Kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019 hazijampa mamlaka yeyote Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa wilaya kuwa msimamizi wa uchaguzi.
WAITARA ameeleza hayo septemba 5 bungeni jijini hapa wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kibamba JOHN MNYIKA aliyehoji sababu ya wakuu wa mikoa na wilaya kupewa mamlaka kwenye usimamizi wa uchaguzi wakati ni makada wa Chama cha Mapinduzi huku akionyesha hofu kuwa uchaguzi huo hautakuwa huru na haki.
Akijibu swali hilo WAITARA amesema uchaguzi huo unasimamiwa na waziri mwenye dhamana na utakuwa huru na wa haki hivyo hawana sababu ya kuwa na hofu.
Uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 unatarajiwa kufanyika novemba 24 huku msisitizo kwa sasa ikiwa ni elimu ya mpiga kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Serikali imesema mpango wa kunusuru kaya maskini umejipanga kuhakikisha malalamiko yaliyokuwepo ya upendeleo,ubaguzi na kuachwa kwa watu maskini kuandikishwa kwenye mpango huo hayajirudii na mifumo ya kielektroniki itatumika.
Hayo yameelezwa leo bungeni jijini Dodoma na naibu waziri ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora MERRY MWANJELWA wakati akijibu swali la mbunge wa Tunduru Kaskazini mhandisi RAMO MAKANI.
MWANJELWA amesema changamoto kubwa ambayo mpango huo umekuwa ukikumbana nao ni kilio kutoka kwa baadhi ya wananchi maskini ambao hawajafikiwa na huduma za mpango huo kwenye vijiji,mitaa na shehia takribani 5,693.
MWANJELWA amesisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa viongozi na watumishi katika ngazi zote ambao katika maeneo yao watabainika kuwepo watu au kaya zisizo na vigezo kwenye awamu ya pili ya mpango huo.
Tags