Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi Mkoani Kagera Revocatus Malimi,alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 12 Majira ya saa 4:40 katika shule ya msingi Kumnazi iliyopo tarafa ya Nyamiaga Wilayani Ngara.
Kamanda Malimi,alisema kamati ya mitihani ya wilaya hiyo ilipata taarifa kuwa baadhi ya walimu watano waliokuwa wamejifungia ndani ya nyumba ya mmojawapo wa walimu hao waliokuwa na mtihani wa sayansi wakiandaa majibu kwa ajili ya kuwapa baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakiendelea na mitihani ya taifa.
Hata hivyo aliwataja walimu wa shule ya msingi Kumnazi wanaoshikiliwa kuwa ni Manase,Mtinange ( 50 ) mkuu wa shule hiyo,Prosper Pius (29),Joachimu Kakuru ( 31 ),Christiana Ilete ( 27 ) na Eric Balbati ( 30 ).
Alisema wasimamizi watano walioteuliwa kusimamia mitihani katika shule hiyo wanaoshikiliwa pia kwa mahojiano ni Revocatus Juhudio ( 37 ) shule ya msingi Kashalazi, Jerusa Mganga ( 46 ) shule ya msingi Nyakahanga Rusumo,Rusalo Izaac maarufu Petro ( 31 ) shule ya msingi Kashalazi, Jofrey Mshahiri ( 31 ) shule ya msingi Mayenzi na Hezron Eugo ( 43 ) msimamizi mkuu wa kituo kizima .
Aidha idadi na majina ya watoto waliokuwa wanaandaliwa majibu ya mtihani na walimu hao imehifadhiwa kwa mujibu wa sheria ya kulinda haki za mtoto.
Vilevile jeshi hilo linaendelea na uchunguzi na uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtihani huo ulipatikana mazingira ya shuleni hapo na kuongezea kuwa kitendo kilichofanywa na watuhumiwa hao ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria.
Aliongezea kwa kusema kuwa mtihani ni siri kuu ya nchi licha ya kupewa semina na kula kiapo cha uadilifu ikithibitika wamehusika na udanganyifu wa aina yoyote wakifikishwa mahakamani adhabu yake ni kubwa.