Wambura ataja lengo la kanuni mpya za mavazi
0
September 05, 2019
Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi TPBL, Boniface Wambura amefafanua juu ya suala la mavazi yanayotakiwa kwa mabenchi ya ufundi ya timu za ligi kuu, linaloendelea kuvuma hivi sasa nchini.
Suala hilo limechukua sura mpya baada ya adhabu ya kwanza juu ya kanuni hizo mpya, iliyotolewa kwa kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye alidaiwa kuvunja sheria kwa kuvaa mavazi ambayo si nadhifu wakati wa mchezo wa kwanza wa ligi baina ya timu hiyo na Ruvu Shooting.
Akielezea kuhusiana na suala hilo, Wambura amesema kuwa halipaswi kuchukuliwa kama ni suala la ajabu au kwa ukubwa kama inavyochukuliwa sasa kwa sababu kanuni zilibadilishwa na klabu zinafahamu, hivyo klabu zinapaswa kufuata utaratibu.
"Uamuzi umefanyika kwa kuzingatia kanuni, bahati mbaya imeanzia kwa Zahera lakini uamuzi uliofanywa na kamati katika mzunguko wa kwanza tu wa ligi ni dalili kwa watu wengine kuwa mambo hayapaswi kuwa hivyo", amesema
"Mabenchi ya ufundi tunatakiwa tuziwakilishe timu zetu na makocha nao wavae mavazi rasmi ili kuonesha heshima ya kazi ya ukocha", ameongeza.
Ikumbukwe kuwa kanuni hizo za mavazi kwa mabenchi ya ufundi zimerekebishwa msimu huu na rungu la kwanza limempata kocha Zahera, ambapo amepigwa faini ya Shillingi laki 5 na adhabu ya kufungiwa mechi tatu mfululizo za ligi.
Tags