Watoto Wawili Wauawa, Kisa? Kujisaidia Hadharani
0
September 27, 2019
MAMILIONI ya raia wa India walio masikini wanaendelea kujisaidia haja kubwa hadharani.
Wanaume wawili katika jimbo la kati la India, Madhya Pradesh, wamekamatwa kwa madai ya kuwaua watoto wawili waliokuwa wakijisaidia haja kubwa hadharani, polisi wamesema.
Roshini, mwenye umri wa miaka 12 na Avinash (10) waliuawa Jumatano wiki hii walipokutwa wakijisaidia haja kubwa karibu na barabara moja kijijini. Familia ya watoto hao ililiambia shirika la utangazaji la BBC Hindi kwamba hawana vyoo nyumbani.
Mamilioni ya raia wa India hujisaidia haja kubwa hadharani, suala ambalo huwaweka watoto na wanawake hatarini.
”Watoto hao wawili walipigwa fimbo hadi kufa. Waliowapiga wamefunguliwa mashtaka ya mauaji,” alisema afisa wa polisi, Rajesh Chandel akiwataja wahusika kuwa ni Rameshwar Yadav na Hakim Yadav.
Familia ya watoto hao imesema imeshindwa kupata ruzuku ya serikali kuhusu mpango wa kuwajengea vyoo watu masikini. Programu ya Swachh Bharat Mission au mpango wa usafi wa India umedhamiria kulimaliza suala la wananchi kujisaidia haja kubwa hadharani na kuimarisha usafi nchini humo.
Wakati Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, alipozindua mpango huo mnamo 2014, aliapa kuifanya India kuwa iondokane na tatizo hilo ifikapo Oktoba 2, 2019.
Tags