Waziri Lugola afurahishwa na bidhaa za asili Tamasha la JAMAFEST Dar
0
September 25, 2019
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema Tamasha la Utamaduni na Sanaa la Nchi za Afrika Mashariki (Jamafest) ambalo linaendelea katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, linapaswa kutangazwa zaidi kwa kuwa bidhaa mbalimbali katika tamasha hilo ni za kipekee.
Waziri Lugola amewataka wananchi kufika kwa wingi katika viwanja hivyo vilivyopo Wilayani Temeke, ili kujionea umuhimu wa bidhaa hizo na kuzinunua ambazo zinatoka katika nchi mbalimbali za Afrika Mashairiki.
Akizungumza wakati alipokuwa anakagua mabanda mbalimbali katika viwanja hivyo, alisema bidhaa za asili zilizopo katika maonyesho hayo, ni za viwango vya juu, na zinapaswa kuungwa mkono na wananchi wa nchi za Afrika Mashariki.
“Nimepita katika mabanda zaidi ya kumi, hakika bidhaa nilizoziona ni nzuri mnoo, na nimezipenda sana ndio mana nimezinunua wakati nilipokua nakagua, hongereni sana waandaji wa tamasha hili,” alisema Lugola.
Aliongeza kuwa, mabanda yapo mengi katika tamasha hilo, waandaaji wamejipanga vizuri kuhakikisha maonyesho hayo yanaenda vema mpaka yatakapomalizika.
Alisema, ametembelea mabanda ya Watanzania, Kenya na Uganda na mengineyo, kujionea jinsi bidhaa mbalimbali za asili zilivyotengezwa, na akagundua kuwa, tamasha hilo linapaswa kuungwa mkono na lifanyike mara kwa mara ili liweze kuunganisha wana Afrika Mashairiki.
Aidha, Lugola alisema tamasha hilo litumike zaidi kukuza lugha yetu ya Kiswahili ambayo ndio inatumika zaidi katika nchi za Afrika Mashairiki.
“Nawapongeza sana Wizara ya Habari na Utamaduni kwa kujipanga na kuleta vitu vizuri kabisa ambavyo vinatufanya tujue tamaduni mbalimbali na kuona bidhaa za asili kutoka katika mataifa mbalimbali, hakika mnapaswa kupongezwa mnoo kwa kufanya kazi nzuri,” alisema Lugola.
Tamasha hilo lilizinduliwa Jumapili Septemba 22, 2019, na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, na linatarajiwa kumalizika Septemba 28, 2019 katika viwanja hivyo.
Tags