Waziri Lugola Asema Serikali Itaendelea Kufuata Misingi Ya Kidemokrasia Kwa Kuzingatia Na Kulinda Haki Za Binadamu.
0
September 27, 2019
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola amesema kuwa serikali ya Tanzania imekuwa ikijidhatiti katika kufuata Misingi ya Kidemokrasia kwa kuzingatia na kulinda na kutetea haki za Binadamu.
Waziri lugola ameyasema hayo Septemba 26,2019 Jijini Dodoma wakati akizindua Ofisi ya kituo cha sheria na haki za Binadamu LHRC,ambapo amesema katika kuyatekeleza hayo kwa vitendo serikali ya Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zenye katiba ambazo ndani mwake zimeonesha bayana masuala ya haki za binadamu na Utawala Bora.
Hata hivyo,waziri lugola amesema serikali imetoa fursa kwa Asasi za kiraia kuanzishwa na kufanya kazi ya kuwajengea wananchi uwezo juu ya masuala mbalimbali ya kiraia ikiwemo sheria , haki za binadamu na uwajibikaji .
Katika hatua nyingine Waziri Lugola amesema ujio wa Kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) Jijini Dodoma ni fursa kwa wanachi wa Dodoma na mikoa ya kanda ya kati kwa ujumla .
Akisoma Hotuba mbele ya Mgeni Rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Bi Anna Henga amesema kituo hicho kimekuwa kikifanya tafiti mbalimbali hususan masuala ya Haki za Binadamu.
Sanjari na hayo Bi Henga amesema kuanzishwa kwa ofisi jijini Dodoma imetokana na msukumo usio zuilika wala kukwepeka wa kudumisha mashirikiano hayo na serikali pamoja na Bunge.
Uzinduzi wa ofisi hiyo unalenga kudumisha mahusiano ya kikazi baina ya taasisi za kiserikali kama vile Bunge na mahakama hasa ukizingatia kuwa taasisi zote za kiserikali zimeshahamia Jijini hapa kufuatia dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Dodoma kuwa makuu ya Nchi .
Kituo cha kisheria na haki za Binadamu ni Asasi ya kiraia isilofungamana na itikadi zozote za kisiasa hivyo imekuwa ikitetea watu wote bila kujali itikadi zozote
Tags