Waziri Mkuu: Wakulima Msiuze Pamba Chini Ya Sh. 1,200


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa zao la pamba nchini wasikubali kuuza pamba yao chini ya bei elekezi ya sh. 1,200.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewashauri wafanyabiashara wa zao hilo waungane na kuanzisha viwanda vya kutengeneza nyuzi na nguo ili kuongeza thamani kabla ya kuuza pamoja na kuwahakikishia wakulima soko.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 21, 2019) wakati akizungumza na viongozi na wananchama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Chato  (CCU) pamoja na wananchi kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha Chato kinachomilikiwa na CCU mkoani Geita.

Amesema wakulima waendelee kuwa na subira kwa sababu wanunuzi hao wamepewa fedha za kutosha kununua pamba yote kwa bei ya 1,200 na si vinginevyo.

“Hata mkiwa na shida msikubali kuuza pamba yenu chini ya sh. 1,200 kwa kuwa haitachukua muda mrefu mtakuwa mmeshapata fedha zenu. Tuna taarifa kuwa kuna wanunuzi wamepata fedha na wanawatumia watu kwenda kuwalaghai wakulima kwa kutaka kununua kwa bei ya sh. 800, msikubali na mkiwaona mtupe taarifa.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema viwanda vya nyuzi na vya nguo vikijengwa nchini vitakuwa na uhakika wa soko kwani hivi sasa Tanzania  haina viwanda vya kutosha vya nguo. Amesema Serikali ipo tayari kuwaunga mkono Watanzania wote au mwekezaji yeyote atakayekuwa tayari kuanzisha viwanda vya aina hiyo kwa sababu mahitaji ni makubwa.

“Tuna shule zaidi ya 18,000 Tanzania na wanafunzi wote wanavaa sare zinatokanazo na pamba, tukisema majora ya sare yasukwe humu humu ndani na kisha kusambazwa mikoa yote bado nguo za watu wanaovaa mitaani. Watapata faida tu.”

Pia, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wote wa vyama vya ushirika katika maeneo yanayolima pamba kuwaelimisha wakulima kuhusu umuhimu wa kuzalisha pamba safi ili walinde heshima ya pamba ya Tanzania ambayo duniani inasifika kuwa ni dhahabu nyeupe.

Awali, Meneja wa CCU, Charles Nyasi alimwambia Waziri Mkuu kuwa makampuni ya METEL, KCCL na FRESHO yamejitokeza kununua pamba kupitia AMCOS na tayari kilo 9,611,860 zimenunuliwa  kati ya kilo 11, 140,529 zilizokusanywa.

Alisema kampuni ya FRESHO imenunua kilo 4, 869, 960, KCCL imenunua kilo 3, 025,051 na METEL imenunua kilo 1,716, 420.

Pia Meneja huyo aliiomba Serikali  isaidie kuwalipia deni la sh. 696,854,475.20 ili kumaliza tatizo la madai ya watumishi na wadai wengine. Pia aliiomba Serikali isaidie kuilipia CCU deni la sh. 102, 942,300.00 la ardhi waliyotumia kujengwa kiwanda chao.

Akijibu maombi hayo Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haiwezi kulipa deni hilo hadi itakapopewa maelezo ya kina ni nani aliyesabaisha deni, mazingira yaliyosababisha deni hilo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad