Yanga wapo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, walilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Zesco United uwanja wa Taifa kisha Azam FC nao wakakubali kupoteza mara ya kwanza uwanja wa Chamazi kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Triangel United.
Mashabiki na baadhi ya viongozi wanaonekana kukata tamaa na timu zao kwa sasa kwenye michuano hii mikubwa inayoandaliwa na Caf ila bado kuna nafasi ya kufanya kuelekea kwenye marudio ya michezo hii ya kimataifa kwa wawakilishi wa Tanzania ambayo inachezwa leo Septemba 28, ni dakika 90 za moto kwa timu zote ila endapo watafanya haya kuna nafasi ya kupenya:-
Kukubali matokeo ya nyumbani
Kwa sasa Azam FC na Yanga hawana namna nyingine ya kufanya zaidi ya kuyakubali matokeo waliyoyapata kwani kuyakataa kutawaongezea ugumu wa kutafuta ushindi kwenye michezo yao ya marudio ni suala la kuamini kwamba walifanya makosa na kupata kile ambacho hawakutarajia.
Itakuwa rahisi kwao kuwapa ugumu wa kupambana na kupata hasira za kutafuta matokeo kwenye mchezo unaofuata endapo watakuwa na imani kwamba hawakustahili kupata matokeo ya mwanzo.
Kuandaa mbinu mbadala
Hapa mabenchi yote ya ufundi yana kazi ya kuandaa mbinu mbadala ambazo zitatumika kuwamaliza wapinzani mapema.Kwa mfano tunaona namna ambavyo Yanga imekuwa ikihaha kutafuta matokeo hasa kwa washambuliaji wake kushindwa kumalizia nafasi ambazo wanazitengeneza huku kwa upande wa Azam FC namna washambuliaji wanavyohaha kupata mipira kutoka kwa viungo.
Kwa timu zote mbili kumekuwa na ugumu wa kutengeneza pasi za umaliziaji hasa wachezaji wanapofika eneo la hatari, ni muhimu kwa benchi la ufundi kulitazama hili kwa ukaribu na kulipa dawa washambuliaji wao wengi wamekuwa wakicheza mithili ya viungo jambo ambalo linawaongezea ugumu kwenye kupachika mabao licha ya kupata nafasi.
Kujiamini
Wachezaji wanakazi kubwa ya kuongeza uwezo wa kujiamini ukizingatia kwamba mechi za marudio wote watakuwa ugenini. Tumeona namna ilivyokuwa shida kwa Idd Chilunda wa Azam FC alitokea benchi baada ya muda mwalimu akaona hajiamini akaamua kumtoa ni pigo kwa wachezaji ambao wanatafuta ushindi kushindwa kujiamini.
Nidhamu nje na ndani ya uwanja
Imekuwa ni kawaida wachezaji wakiwa nyumbani kuwadharau wapinzani jambo ambalo huongeza wepesi kwa wapinzani kushinda kwa nafasi ambayo ipo mbeleni kwa wawakilishi wetu kimataifa ni dhahiri kwamba mkiwaheshimu wapinzani wenu ugenini ni fursa kwenu kutusua.
Tumeskia Kocha wa Zesco United, George Lwandamina akisema kuwa ni ngumu kwake kupoteza nyumbani, tayari kuna ukuta amejiwekea ambao ni kujiamini hapo ndipo pakuanzia kupanda kabla ya kutusua ugenini.
Kutobweteka na matokeo yaliyopita
Azam FC na Yanga zote mbili kwenye michezo yao ya kimataifa zilipata aina moja ya matokeo sawa na waliyoipata kwa sasa kwenye michezo yao ya awali , Azam ilipoteza mbele ya Fasil Kenema ugenini na Yanga ililazimisha sare mbele ya Township Rollers nyumbani na mwisho wa siku wakapindua meza kibabe.
Ushindi ambao waliupata mbele ya Fasil Kenema na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2 usiwape kiburi Azam na kubweteka wakiamini miujiza wala Yanga ushindi wao wa bao 1-0 na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 mbele ya Township Rolers usiwape kiburi hatua ya sasa ni ngumu kuliko ile ya awali.
Juhudi isiyo ya kawaida
Timu zote kwa sasa zinapaswa zitambue kuwa juhudi zao ndani ya uwanja ndizo zitakazowapa matokeo chanya. Wasijisahau pale watakapopata bao la mapema bali ni muda wa kujipanga upya kwa kuongeza juhudi upande wa kujilinda na kushambulia.
Kutafuta majibu sahihi ya anguko lao
Kwa mfano Yanga ambao walianza kushinda mapema walipoteza nguvu nyingi kufurahia ushindi walioupata na kusahau kwamba mpira unaendelea na mwisho wa siku wakawapa nafasi wapinzani. Azam wao ilikuwa ngumu kushinda baada ya kufungwa bao la mapema timu ilipoteana na kila mchezaji akawa anacheza anavyojua.
Udhaifu wao kimataifa upo hapa
Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema kuwa waliponzwa na uchu wa wachezaji kutafuta magoli mengi zaidi jambo lililowapa nafasi ya kufunguka zaidi na kujisahau kuweka ulinzi langoni.
“Tulifunga bao la mapema kipindi cha kwanza, wachezaji wakawa wanahaha kutafuta bao lingine la pili kujiweka kwenye nafasi nzuri na kusahau kujilinda jambo lililowapa nafasi wapinzani wetu kutufunga,” alisema.
Etienne Ndayiragije, Kocha Mkuu wa Azam FC alisema kuwa kushindwa kujiamini kwa wachezaji wake kumemfanya akose matokeo kimataifa anajiandaa kwenda kupindua meza ugenini.