KESHO Jumamosi ndiyo siku ya balaa lenyewe wakati Yanga itakapoingia uwanjani kukipiga na Zesco United ya Zambia, mchezo ambao vazi lake rasmi litakuwa ni pensi.
Yanga na Zesco wanacheza mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ni wa kwanza wa raundi ya kwanza katika mashindano hayo msimu huu.
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema, yuko tayari kwa mchezo huo na imani yake watawang'oa Zesco.
"Zesco ni timu kubwa na kongwe katika mashindano haya makubwa hivyo tunatakiwa kucheza nao kwa akili kuona tunaibuka na ushindi,"alisema Zahera.
BALAMA AONGEZEWA MAJUKUMU
Zahera amekuwa akimtengeneza winga wake, Mapunduzi Balama kuwa na msaada kwenye safu ya ulinzi wa beki ya kulia kutokana na mapungufu aliyonayo kikosini.
Mapinduzi ambaye kiuhalisia anacheza nafasi ya winga na Zahera amekuwa akimtumia zaidi kucheza winga wa kulia, hivyo kutokana na mpango huo itabidi afanye kazi ya kukaba.
Hii ni kutokuwa fiti kwa wachezaji wake, Juma Abdul ambaye amejiunga na timu hivi karibuni alipata matatizo ya kifamilia alipofiwa na mama yake mzazi wakati, Paul Godfrey anasumbuliwa na goti huku Mrundi Mustapha Selemani bado hajapata ITC.
Abdul amejiunga na timu siku mbili zilizopita na kabla Zahera alikuwa akimtumia Mustafa katika mechi za kirafiki na mashindano ambaye kiuhalisia ni beki wa kati.
Hivyo katika mchezo wa kesho wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa dhidi ya Zesco United ya Zambia, Mapinduzi huenda akawa na majukumu mengi uwanjani, mbali na kucheza nafasi ya winga, itambidi amsaidie zaidi Mustapha.
"Imebidi kumtumia zaidi Mapinduzi kucheza nafasi yake lakini anakuwa nyuma zaidi kama beki (wingback) kwa ajili ya kutoa msaada kwenye ulinzi kama unavyojua tuna mapungufu kwenye nafasi hiyo,"lisema Zahera.
Alisema, ameona Mapinduzi anafaa kutokana na kasi yake ya kushuka na kupandisha mashambulizi kwa nguvu.
Hii ilijionyesha katika mazoezi yao waliyofanya kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana Alhamisi.
"Kama ulivyoona wachezaji wanaocheza nafasi hiyo wana matatizo ndiyo maana ninamjaribu yeye."