LEO fanya hivi, angalia mechi ya Liverpool na Newcastle kwa kipindi kimoja tu, baada ya hapo nenda Uwanja wa Taifa kuwasapoti wakimataifa, Yanga watakapokuwa wakicheza na Zesco ya Zambia.
Yanga leo Jumamosi inakuwa mwenyeji wa Zesco kwenye mchezo wa Hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mshindi wa jumla atakwenda moja kwa moja hatua ya makundi ya michuano hiyo na akitolewa atakwenda kucheza playoff Kombe la Shirikisho.
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, amekuwa akikiandaa kikosi chake kwa muda mrefu ikiwemo kwenda kuweka kambi jijini Mwanza ambako walicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Pamba na Toto Africans.
Sasa baada ya kurejea Dar juzi, Yanga juzi na jana walifanya mazoezi ya mwishomwisho kwa ajili ya mchezo huo huku Zahera akitamka kuwa kazi imekwisha na Zesco lazima wapigwe.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Zahera alisema kuwa licha ya wapinzani wao kuwa na uzoefu mkubwa na michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa lakini dakika 90 ndizo zitaamua kati yao huku akiwa na uhakika mkubwa wa kushinda.
Kocha huyo ameongeza kwamba tayari ana siri zote za Zesco United inayofundishwa na George Lwandamina kutokana na kutumiwa ‘CD’ na kocha wa TP Mazembe, Mihayo Kazembe walipocheza nao.
“Najua Zesco wamecheza mechi nyingi za kimataifa na wana uzoefu kuliko sisi, lakini mpira wa sasa ni dakika 90, yule ambaye yuko tayari kiakili ndiye ambaye anapata matokeo.
“Wao wana wachezaji wazuri na uzoefu kweli zaidi yetu lakini hilo halitusumbui na uzuri ni kwamba nawajua wote, nimepata vitu vyao vingi hata kocha wa TP Mazembe alinitumia ‘CD’ walipocheza nao kwa hiyo itanisaidia.
“Wao ninawajua na sisi wanatujua, lakini hilo haliwezi kutuzuia kufanya kile tunachokitaka. Uzuri ni kwamba nina wachezaji wangu wote isipokuwa wawili tu, Paul Godfrey (Boxer) na Issa Bigirimana ambao wana majeruhi, lakini wote waliobakia wapo vizuri na wanaweza kucheza mechi hiyo,” alisema Zahera.
CAF KUIJAZA BILIONI
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika ‘Caf’ timu itakayofanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo itapatiwa donge nono la dola 550,000 (zaidi ya Sh 1.5 bilioni).
Kocha wa Yanga, Zahera ameonyesha kuwa na nia ya dhati kuiongoza timu hiyo kuhakikisha inachukua kitita hicho ambacho kitawasaidia katika mambo mbalimbali.
“Fedha hizo ni nyingi, hakika kama tutafanikiwa kutinga hatua ya makundi na kuzipata kwa namna moja ama nyingine tutakuwa tumepiga hatua katika suala zima la uchumi.
“Kwa hiyo kila mchezaji anatakiwa kupambana vilivyo hiyo kesho (leo), ili tuweze kupata ushindi,” alisema Zahera na kuongeza:
“Kuhusiana na wachezaji watakaoanza hiyo ni siri yangu lakini kuna uwezekano nikatumia mfumo wa 3-5-2 kutokana na Boxer kuwa majeruhi.”
Kikosi cha Yanga ambacho leo kinaweza kuanza kitakuwa hivi; kipa, Faruk Shikalo, Lamine Moro, Kelvin Yondani, Ally Mtono ‘Sonso’, Papy Tshishimbi, Abdulaziz Makame, Mohamed Issa ‘Banka’, Mapinduzi Balama, Patrick Sibomana, Juma Balinya na Sadney Urikhob.
WAAMUZI HAWA HAPA
Mwamuzi wa kati anatarajiwa kuwa Helder De Calvalho ambaye atasiadiwa na Jerson Do Santos na Ivanildo Lopes wote kutoka Angola huku kamishna wa mchezo anatarajiwa kuwa Gaspard Kayijuka kutoka Rwanda.
MJAPAN WA ZESCO GUMZO
Kiungo wa Zesco, Kosuke Nakamachi ambaye ni raia wa Japan amekuwa gumzo jijini Dar tangu atue huku mashabiki wengi wakionekana kutaka akumuona akiichezea timu yake hiyo leo.
Kundi kubwa la mashabiki waliokuwa wakielekea Uwanja wa Uhuru, Dar jana jioni ambako Simba ilikuwa ikicheza na Mtibwa, lilikuwa likitaja jina la nchi anayotokea mchezaji huyo kwa kuwa hawakuwa wakilijua jina lake na namna ya kulitamka.