Yote yaliyojiri katika mazungumzo ya Rais Magufuli na Nape Nnauye



Mbunge wa Jimbo la Mtama Mkoani Lindi, Mhe. Nape Nnauye amekutana na kumuomba radhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kufuatia kuhusika kwake katika mazungumzo yasiyofaa dhidi ya Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Nape Nnauye amekutana na Mhe. Rais Magufuli leo tarehe 10 Septemba, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo, Mhe. Nape amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukubali ombi lake la kukutana nae na kumsikiliza, na pia kumsamehe kwa makosa aliyoyafanya kufuatia taharuki iliyoibuka baada ya kuvuja kwa sauti za mawasiliano yake na wanasiasa wengine wakimsema Mhe. Rais Magufuli.

“Kwa hiyo baada ya kupata fursa nimekuja nimemuona, na mle ambamo nilimkosea kama Baba yangu nimeongea nae na Baba amenielewa, ameniambia amenisamehe na amenipa ushauri ambao nitaufanyia kazi na naamini baada ya hapa mambo yatakwenda vizuri, na kwa kweli kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru sana sana, amenipa fursa kubwa, ndefu na ameongea maneno mengi kwangu na ushauri wake nimeuchukua” amesema Mhe. Nape Nnauye.

Kuhusu maendeleo, Mhe. Nape Nnauye amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali na amesema ana matumaini kuwa CCM itapata ushindi katika chaguzi kutokana na kazi hiyo.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli amesema Mhe. Nape amekuwa akiomba kukutana nae mara nyingi na tangu siku nyingi kupitia kwa watu mbalimbali wakiwemo wasaidizi wake, viongozi wastaafu na viongozi wa CCM, na kwamba baada ya kukutana nae na kumuomba radhi ameamua kumsahehe.

Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mhe. Nape Nnauye kwenda kufanya kazi za kuhudumia wananchi wa Jimbo lake la Mtama na kukitumikia vyema chama chake cha CCM.

“Yote nimesamehe, huyu bado ni kijana mdogo, ana matarajio makubwa katika maisha yake, mimi nikiendelea kumshikilia kwenye moyo wangu kwanza ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu na tumefundishwa katika maandiko yote tusamehe saba mara sabini, kwa hiyo nimemsamehe na Mungu amsaidie katika shughuli zake akafanye kazi zake vizuri, akalee Mke wake na familia yake, akakitumikie chama, akawatumikie wananchi wa Jimbo lake vizuri, mimi nimemsamehe, labda kama yeye atakengeuka hiyo itakuwa ni juu yake, lakini mimi kutoka moyoni mwangu nimeshamsamehe na nimemsaheme kweli. Nape nenda ukafanye kazi, Mungu akujaalie” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad