Asilimia 25 ya mazao Duniani yanaathiriwa na sumukuvu
0
October 17, 2019
Kwa miaka ya hivi karibuni kumejitokeza changamoto ya chakula salama (Safe food) kutokana na uwepo wa tatizo la sumukuvu katika mazao ya chakula, hususani mahindi na karanga ambayo huchangia upatikanaji wa lishe bora na ni chakula muhimu kwa Watanzania walio wengi.
Taarifa zinaonesha kuwa tatizo la sumukuvu ni kubwa kwani inakadiriwa kuwa asilimia 25 ya mazao yote yanayozalishwa duniani yanaathiriwa na sumukuvu. sumukuvu ina athari kubwa za kiafya na huchangia karibu asilimia 30 ya saratani ya ini, kuharibu mfumo wa kinga na kupelekea udumavu kwa watoto.
Hayo yamebainishwa na waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga jana, wakati akifunga maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani mwaka 2019 ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Bombadier mkoani Singida.
Amesema kuwa athari hizi haziishii tu kwa binadamu, bali hata mifugo nayo huathiriwa na tatizo hili, hivyo kupelekea mtu kula sumu hizi kupitia mazao ya wanyama kama vile maziwa, mayai, samaki na nyama kutoka kwa wanyama waliolishwa vyakula vyenye sumukuvu kwa kiwango kikubwa.
Mazao hayo pia yana umuhimu mkubwa katika kupata lishe bora, hivyo ametoa mwito kwa wafugaji wote nchini kuchukua tahadhari dhidi ya sumukuvu katika sekta ya mifugo ili kutekeleza kaulimbiu ya maadhimisho haya kwa vitendo.
Kadhalika amesema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufi kupitia wizara ya kilimo hivi karibuni ilizindua mkakati maalumu wa kupambana na sumukuvu nchini hivyo wananchi wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo za serikali.
Amesema kuwa Madhara ya Sumukuvu si tu huchangia upotevu wa nguvukazi na kudumaza akili za watoto bali pia hupunguza tija na kipato kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. “Kama tunavyokumbuka mwaka 2016, watu 68 katika Halmashauri za Bahi, Chemba, Kiteto na Kondoa waliugua baada ya kula chakula chenye kiwango kikubwa cha sumukuvu na watu 19 kufariki dunia kutokana na tatizo hilo” Amesema Hasunga
Amesisitiza kuwa ili kupata lishe bora na ulimwengu usio na njaa, serikali haina budi kushughulikia changamoto hizi kwa ujumla wake ili kuendana na kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya chakula Duniani mwaka 2019 isemayo Lishe bora kwa ulimwengu usio na njaa, kwani ina maana kubwa sana katika kuhakikisha si tu tunazalisha chakula cha kutosheleza mahitaji lakini tunahitaji chakula kilicho salama ili kuboresha lishe na afya za wananchi wetu.
“Kama tunavyokumbuka mnamo mwezi Machi mwaka 2019, nilizindua Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu Nchini (TANIPAC) ambao una lengo la kupunguza sumukuvu (aflatoxin) katika mazao ya mahindi na karanga. Hivyo, naamini mafanikio ya mradi huu yatachangia sana katika kuimarisha lishe na kuongeza upatikanaji wa chakula bora na salama hapa nchini. Nirudie kuagiza tena watendaji wa Wizara kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huu ikiwemo elimu kwa wananchi ili kuepuka madhara ya sumukuvu, na hivyo kuimarisha lishe kwa watu wa rika zote” Alisisitiza Waziri Hasunga.
Aidha amewataka Wataalamu wa sekta ya kilimo kutafuta namna bora ya kuhakikisha Tanzania inaondokana na tatizo la lishe duni kwa kaya kwani Tanzania inazalisha chakula kwa wingi na cha kutosha. “Nchi yetu haina njaa na tutaendelea kusimamia uzalishaji kwa kutoa kipaumbele kwa upatikanaji wa pembejeo na viuatilifu vyenye bei nafuu na kuhakikisha masoko ya mazao ya wakulima yanapatikana”
Tags