Bodi ya Ligi yafungukia Magori kumrithi Wambura
0
October 19, 2019
BODI ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPBL), imefungukia madai ya aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Cresentius Magori kutaka kurithi nafasi ya Boniface Wambura katika nafasi ya utendaji mkuu wa bodi hiyo.
Magori ambaye alikuwa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, amekuwa akihusishwa kurithi nafasi ya Wambura ambaye mkataba wake umeisha, hivyo kuwepo na mchakato wa kumsaka mrithi wake.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mgutto, alisema wapo tayari kumpokea Magori kama ilivyo kwa wadau wengine wa soka watakaopendezwa na kuwania nafasi hiyo pindi mchakato utakapoanza na si kama inavyoelezwa kuwa ameandaliwa kurithi nafasi hiyo.
“Ndani ya siku mbili hizi tunatarajia kutoa tangazo la nafasi za kazi kwa ajili ya kutafuta mrithi wa Wambura ambapo kuna vigezo mbalimbali vinatakiwa kuwepo kwa mgombea anayehitaji kuwania nafasi hiyo, lengo ni kuwa na kiongozi bora.
“Kuhusu suala la Magori nimekuwa nikisikia kutoka kwa watu mbalimbali kuwa ndiye aliyepangwa kurithi nafasi ya Wambura lakini si kweli, ila iwapo atahitaji kuwania nafasi hiyo ni vyema akawasilisha CV ‘wasifu’ yake kama ilivyo kwa wadau wengine watakaojitokeza kuomba nafasi hizo kulingana na vigezo vitakavyotolewa ili kumpata mtendaji mpya,” alisema Mgutto
Tags