CCM Yawaonya Viongozi Wanaotoa Siri za vikao


Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Phillip Mangula amewaonya viongozi wanaotoa siri za vikao, kwani kufanya hivyo ni kukiuka maadili.

Mangula ametoa onyo hilo mkoani Simiyu wakati wa mkutano wa Halmashauri ya CCM ya wilaya na mkoa na watendaji wa serikali wa halmashauri sita za wilaya za mkoa wa Simiyu.</p>

Amesema viongozi wanaotoa siri za vikao hawafai kuongoza chama na wanapobainika ni vema wakachukuliwa hatua za kinidhamu.

"Kumekuwa na tabia chafu kwa baadhi ya viongozi ndani ya chama chetu ambao wanatoa siri za ndani za vikao...na kama hamjui kufanya hivyo ni kukiuka kanuni za chama na kama kuna viongozi watakaobainika kufanya hivyo wachukuliwe hatua za nidhamu," amesema.

Ameagiza viongozi wa chama na serikali wazingatie taratibu na kanuni za utendaji wa majukumu yao na kuacha majungu ndani ya ofisi zao ili kuondoa migongano na migogoro.

Alionya pia tabia ya baadhi ya viongozi wa chama kutumia madaraka yao kubughudhi watendaji wa serikali na kuupongeza Mkoa wa Simiyu kwa ujenzi shule bora na zahanati.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amemhakikishia Mangula ushirikiano na chama ili kutimiza maono ya Rais John Magufuli na kuwaomba watendaji kuzidisha kasi ya kusikiliza malalamiko ya wananchi.

Mwenyekiti wa Wilaya ya Maswa, Paul Jidai amesema viongozi wengi wamekosa mafunzo ya uongozi ndio maana huwa wanakosa uadilifu.

Jidai alisema ni vema chama kikawapeleka viongozi katika mafunzo ya uongozi ili waendane na uhalisia wa nafasi wanazopata.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad