Msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Harmonize amesema kuwa tofauti za kibiashara zilizopo kwenye Media za hapa Tanzania zinaua muziki wa Bongo Fleva kwani zinawagawa wasanii na kuwaweka kwenye makundi.
Harmonize akiongea kwenye kipindi cha XXL cha Clouds FM amesema kuwa bifu la Media hizo limepelekea baadhi ya wasanii wenye vipaji kushindwa kutumia fursa za kutumbuiza kwenye majukwaa mbalimbali ya matamasha makubwa kama Fiesta na Wasafi Festival.
“Katika kitu kinachorudisha chini muziki wetu ni tena kwa kasi sana, Ni ugomvi baina ya Media kwa Media. Kwa sababu sasa hivi msanii kabla hajatoka anawaza niende upande gani? akienda huku atabaniwa, Akienda huku atabaniwa. Kuna wasanii wengi wazuri wametoka lakini wanaishi mazingira magumu sana, inatakiwa tukae chini na tuyamalize“amesema Harmonize na kuwatolea mfano Marioo na Whozu.
“Nakupa mfano ulio hai kuna mtu anaitwa Whozu, Ana kipaji na ametoka lakini yupo katikati anawaza aende wapi?.. Achana na Whozu tu kuna mtu Marioo pia ana kipaji lakini ni watu walio kwenye wakati mgumu. Watu kama hawawezi kuja kukwambia ila mimi msanii na wale wasanii wenzangu najua wakati walionao. Natamani sana kuona Media zinafanya kazi kwa pamoja, Inawezekana kabisa msanii wa Tanzania au Kenya akajaza ukumbi London kama wasanii wa Nigeria wanavyofanya kwa sababu tuna nafasi kubwa na tunatumia kiswahili. Lakini hatuwezi kwa sababu sisi wenyewe tunavutana huku chini.“amesema Harmonize.
Kwa upande mwingine, Harmonize amesema kuwa hata yeye baada ya kujitoa kwenye lebo ya Wasafi kwa sasa hana mawasiliano mazuri na timu yake ya zamani ya WCB.