KOCHA na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amefunguka kuwa hana imani kabisa na Yanga kama itashinda mbele ya Pyramids FC kwa kuwa hawako kwenye kiwango kizuri tangu msimu umeanza.
Yanga imepangwa kucheza na Pyramids FC ya Misri ambapo mchezo wa kwanza itacheza Oktoba 27 kisha marudiano Novemba 3, mwaka huu.
Hii ni baada ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuchezesha droo ambapo michezo ya mtoano imepangwa kuwania kufuzu Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Julio alisema: “Ukweli sina imani na Yanga, sababu kiwango chao kwa sasa siyo bora wanashindwa tu kutamba mbele ya Ruvu sijui Coastal ndiyo wakapambane na hao Pyramids, sidhani kama watafanikiwa kwa hilo.
“Yanga kwa sasa ina wachezaji lakini hawana muunganiko, timu haijawa sawa kabisa kusema inaenda kushindani na Mwarabu ambao kwa fitina ndiyo sehemu yao, siyo rahisi kwa wao kusonga mbele, niwe muwazi tu.
“Pia wanatakiwa kuweka mambo yao sawa hasa yale ya ndani, kuvurugana waache, zaidi wapambane kujenga timu ambayo itakuwa inaeleweka wakisema hii ni Yanga hujiulizi mara mbili,” alisema Julio.
Yanga ilitolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika katika Raundi ya Kwanza dhidi ya Zesco United kwa jumla ya mabao 3-2.