Kabudi: Hakuna Mwenye Uwezo wa Kubadili Ukomo wa Rais wa Awamu Mbili
0
October 11, 2019
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema hakuna mtu yoyote mwenye uwezo wa kubadili ukomo wa urais wa awamu mbili huku akisisitiza hilo haliwezekani katu.
Profesa Kabudi amesema hayo jana wakati akifungua kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere ambapo mada kuu ilikuwa inasema miaka 20 baada ya Mwalimu.Profesa Kabudi alikuwa amemuwakilisha Rais Dk.John Magufuli ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.
Wakati anatoa hotuba yake Profesa Kabudi alisema kuwa hakuna wa kubadili awamu mbili za uongozi wa urais."Tutaendelea na vipindi viwili vya ukomo wa urais, na kesi iliyofungulia na moja ya raia wa Tanzania kuhusu ukomo wa Rais, isihusishwe na Rais wa sasa."
Alifafanua kwamba vipindi vya urais ni sehemu ya tunu iliyoachwa na Mwalimu Nyerere na hivyo kila mmoja wetu analojukumu la kuilinda tunu hiyo ambayo imeweka utaratibu mzuri kuhusu ukomo wa Rais.
Profesa Kabudi ametumia nafasi hiyo kuelezea pia uamuzi wa Mwalimu Nyerere katika mfumo wa vyama vingi ambao aliuruhu lakini katika mfumo wa kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na umoja, amani na mshikamano.
Ambapo katika eneo hilo la vyama vingi mbali ya kuwa sehemu ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, ametumia kuhimiza Watanzania wa kada mbalimbali kusoma sheria mpya ya vyama vya siasa ambayo kwa sehemu kubwa imefanyiwa marekebisho.
"Moja ya marekebisho ndani ya sheria ya vyama vingi, inazungumzia umuhimu wa vyama vya siasa kufanya uchaguzi za ndani kwa ajili ya kubadilishana uongozi na wanawake kushirikishwa.
"Pia katika sheria hiyo imezungumza kwa kina suala la uwazi kuhusu vyanzo vya fedha pamoja na matumizi yake ambayo yanatakiwa kuwa wazi na kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.Pia sheria hiyo inapiga marufuku kuwa na vyama vya siasa vyenye muelekeo wa udini, kuligawa taifa na fujo na kueneza chuki miongoni mwetu,"amesema Profesa Kabudi.
Aliongeza kuwa sheria hiyo pia inatoa maelekezo mafunzo na itikadi zinazofundishwa ndani ya vyama vya siasa lazima Msajili wa Vyama vya Siasa apewe taarifa na kushiriki kwenye mafunzo hayo.
Profesa Kabudi wakati anazungumzia mambo ya kumuenzi Mwalimu Nyerere amegusia suala la utaifa na hasa katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inaunganisha wananchi wote bila kujali makabila zaidi ya 120 yaliyopo nchini.
"Kuna mambo mengi ambayo nchi yetu inaendelea kufanya kama sehemu ya kuenzi misingi ambayo wengine wanaita tunu iliyoachwa na Mwalimu Nyerere.Hata hivyo Rais wetu Dk.Magufuli kuna mambo mengi anafanya kwa ajili ya kumuenzi kwa vitendo Mwalimu Nyerere,"amesema Profesa Kabudi.
Alitaja baadhi ya mambo ya hayo ni utekelezwaji wa miradi mikubwa nchini ambayo inafahamika kama miradi ya kimkakati ukiwemo uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano kuhamia rasmi Dodoma kwani huo ulikuwa mpango wa Mwalimu lakini hakufanikiwa kuutekeleza.Pia ujenzi wa mradi wa umeme katika bwawa la Mto Rufiji ambalo kwa sasa linafahamika kama Mwalimu Nyerere Hydro Power Project utakaozalisha megawati 2115 na utagharimu zaidi ya Sh.trilioni 7 fedha ambazo ni za ndani.
Pamoja na hayo Profesa Kabudi amezungumzia ujenzi wa reli ya kisasa ambayo awamu ya kwanza ya ujenzi imeanza Dar es Salaam hadi Dodoma."Mwalimu Nyerere aliwapenda sana Watanzania na hivyo alikuwa na ndoto ya kuona wanakuwa na uchumi wa kati , hivyo Rais Magufuli ameibeba ajenda hiyo kwa vitendo ambapo ndani ya miaka minne ya uongozi wake amehakikisha amejenga na anaendelea kujenga miradi mbalimbali ya kimandeleo.
"Na katika hilo Serikali imeamua kwa vitendo kuboresha huduma za afya kwa kujenga vituo 352 na kwa ujenzi wa kila kituo umegharimu Sh.milioni 500 tofauti na hapo awali ambapo gharama za ujenzi zilikuwa kubwa sana na mkapaka sasa kuna maombi ya ujenzi wa viwanda nane vya dawa nchini,"amesema.
Ameongeza kuwa katika kumuenzi Mwalimu Nyerere ambaye alihakikisha watu wake wanapata elimu, Rais Magufuli ameamua kutoa elimu bure huku akifafanua kuwa kama Watanzania wanakumbuka Rais baada ya kuapishwa alikaa miezi mitatu bila ya kuwa na baraza la mawaziri ili fedha za kuwalipa zitumike kusomesha watoto.
"Uamuzi wa Rais kutoa elimu bure, umeongeza idadi ya uandikishwaji wa wanafunzi kwa asilimia 20.1 .Hali hiyo imeongeza pia idadi ya watoto wanaojiunga na masomo ya sekondari,"amesema Profesa Kabudi.
Katika eneo la maji Profesa Kabudi amesema kuwa ni moja ya changamoto kubwa lakini Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wake wanapata maji safi na salama.
"Nilikuwa kwenye ziara ya Rais, tukiwa huki tumekutana na changamoto ya uhaba wa maji.Nakumbuka siku za karibuni nilikuwa Marekani ambako huko nilikuwa nalala kwenye hoteli ya hadhi ya nyota tano lakini baada ya kurudi na kuungana na Rais kwenye ziara nimelala gesti ya kawaida ambayo maji ya kuoga tunateka kwa ndoo,"amesema.
Kuhusu mikataba Profesa Kabudi amesema kuwa iliyopo sio kwamba haikuwa halali lakini Rais Magufuli kwa mapenzi mema aliyonayo kwa wananchi wake ameona ni vema ikapitiwa ili kuleta tija kwa watu wote tofauti na awali.
"Ndio maana Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kupitia upya mikataba ya madini na leo hii wote tunaona faida yake.Pia mkataba wa Kampuni ya simu ya Airtel ambao umepitiwa upya na sasa tunanufaika na uwepo wa kampuni hiyo.Niwaambie tu pamoja na Serikali kuwa na hisa bado kila mwezi tunapata Sh.bilioni moja kutoka kampuni hiyo na itakuwa hivyo kwa kipindi cha miezi 60,"amesema Profesa Kabudi.
Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuenzi mambo ya msingi ambayo yameachwa na Mwalimu Nyerere kwa maslahi ya Taifa letu la Tanzania
Tags