Kasi Ya Usikilizaji Mashauri Imemaliza Mrundikano Wa Kesi Mahakamani


KATIKA nchi inayoazimia kuwa na uchumi unaokuwa kwa kasi, ni lazima migogoro inayowasilishwa Mahakamani ikamilike kwa haraka ili kuwawezesha wananchi watumie muda wao mwingi katika uzalishaji mali.

Kumekuwa na dhana kuwa mashauri ya jinai na madai yanapochelewa kukamilika mahakamani, basi ni mahakama tu ndiyo inayochelewesha utoaji haki pasipo na kuelewa kuwa katika mnyororo wa utoaji haki kuna wadau muhimu wanaopaswa kutimiza wajibu wao kwa wakati.

Wadau hao ni pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Ofisi ya Taifa ya Mashtaka/DPP, Jeshi la Polisi, Mkemia Mkuu wa Serikali, Jeshi la Magereza, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Tume ya Kurekebisha Sheria (LRC).

Wengine ni pamoja na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kamishna wa Kazi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Serikali ni wadau muhimu na wezeshi kwa Mahakama na utoaji haki ambao wamekuwa wakishirikiana kwa karibu zaidi na wananchi kwa kuhakikisha kuwa wanafuata taratibu za kimahakama za uendeshaji mashauri, wanahudhuria Mahakamani kadri wanavyoitwa pamoja na kukata rufaa ndani ya muda uliowekwa kisheria.

Hatua zote hizi zitasaidia Mahakama kuwahudumia kwa wakati, na kwa ubora zaidi pamoja na kuwahimiza wananchi  kuwa na jukumu la kufahamu taratibu za sharia ikiwemo hatua za mwanzo zinazopaswa kufahamika na mwananchi katika kufungua shauri Mahakamani na kuhakikisha kuwa  anafahamu hatua zote kesi yake itapitia katika ngazi ya Mahakama zote hadi Mahakama ya Rufani.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020 Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Augustine Mahiga anasema  kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani ni ni moja ya vipaumbele muhimu vya Serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata haki sawa na kwa wakati.

Anaongeza kuwa katika kufanikisha azma hiyo, Mahakama ya Tanzania  mwaka 2018 ilianza ikiwa na jumla ya mashauri 65,223, na kusajili mashauri mapya 259,476 katika ngazi zote za Mahakama, ambapo mashauri 255,836 yalitolewa uamuzi ikiwa ni sawa na asilimia 99 ya mashauri yote yaliyofunguliwa katika kipindi hicho.

Dkt. Mahiga anaongeza kuwa mashauri yaliyobaki mahakamani ni 68,863 na kati ya hayo, mashauri yenye umri zaidi ya miaka miwili (mashauri ya mlundikano) ni 3,435 sawa na asilimia 5 tu ya mashauri yote yaliyobaki.

Kwa mujibu wa Waziri Mahiga anasema Kwa ngazi ya Mahakama ya Rufani, mwaka 2018 ulianza na mashauri 2,933 na kusajili mashauri mapya 1,499 ambapo mashauri 1,184 yalisikilizwa na kutolewa uamuzi, sawa na asilimia 79 ya mashauri yote yaliyosajiliwa katika kipindi hicho na mashauri yaliyobaki mahakamani ni 3,248.

’Bila shaka, ongezeko la idadi ya majaji wa Mahakama ya Rufani baada ya uteuzi wa hivi karibuni wa majaji 6 wa mahakama hiyo litasaidia kuharakisha usikilizaji wa mashauri ikilinganishwa na miaka iliyopita’ anasema Waziri Mahiga.

Waziri Mahiga anasema katika ngazi ya Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Kanda na Divisheni, mashauri yaliyokuwepo ni 19,207 na mashauri mapya yaliyosajiliwa ni 18,284 na mashauri yaliyoamuliwa katika kipindi hicho ni 17,046, sawa na asilimia 93 ya mashauri yaliyosajiliwa wakati mashauri yenye umri wa miaka miwili na zaidi ni 1,860 sawa na asilimia 6 ya mashauri yaliyobaki, yakiwemo mashauri 100 yenye miaka 5 na zaidi.

Akifafanua zaidi Waziri Mahiga anasema kwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, zilianza mwaka 2018 na mashauri 24,840 na kusajili mashauri mapya 51,161 ambapo jumla ya mashauri 47,089 yalimalizika, sawa na asilimia 92 na kubakiwa na mashauri 28,912, yakiwemo mashauri 837 yenye umri wa kati ya mwaka mmoja na miaka miwili.

‘Mahakama za mwanzo nchini ndizo zinazoongoza kwa kufungua na kusikiliza idadi kubwa ya mashauri kuliko mahakama za ngazi nyingine ambapo katika mwaka 2018 mahakama hizi zilianza na mashauri 15,055 na kusajili mashauri mapya 177,566’ anasema Waziri Mahiga.

Kwa mujibu wa Waziri Mahiga anasema Mashauri yaliyomalizika ni 176,542 sawa na asilimia 99, na kubakia mashauri 16,079 tu kwa nchi nzima na kati ya mashauri 16,079 yaliyobaki, mashauri ya mlundikano yaliyokuwa na zaidi ya miezi 6 Mahakamani kwa ukomo wa Mahakama hizi ni tisa ambayo yapo katika wilaya za Babati (1), Muleba (6) na Tarime (2).

Aidha Waziri Mahiga anasema katika kuimarisha utawala bora, maadili na uwajibikaji wa watumishi, Mahakama ya Tanzania ilifanya ukaguzi wa huduma za kimahakama katika kanda zote 14 za Mahakama Kuu na kuhusisha vituo 839 vya mahakama.

Anazitaja Mahakama hizo ni pmaoja na Mahakama za mwanzo, mahakama za wilaya na Mahakama Kuu kati ya vituo 980 vilivyopo nchini, sawa na asilimia 86 ikiwemo Vituo vya Mahakama za Mwanzo 717 841 sawa na asilimia 85, Mahakama za Wilaya 97 kati ya Mahakama 111, sawa na asilimia 89 na Mahakama za Hakimu Mkazi vituo 25 kati ya 28 sawa na asilimia 89.

‘Aidha, jumla ya malalamiko 1,046 ya wananchi yanayohusu kero za upatikanaji wa huduma mbalimbali za mahakama yalipokelewa ambapo malalamiko 951, sawa na asilimia 91 yalishughulikiwa’ anasema Waziri Mahiga.

Wadau wa Mahakama wakimaliza wakitimiza wajibu wao kwa wakati, wanaiwezesha mahakama kumaliza mashauri na mwanachi kupata haki yake kwa wakati sambamba na wananchi kusoma sheria ili angalau wawe na uelewa ili kutowaachia wanasheria peke yao jukumu la kufahamu taratibu za sheria.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad