Kauli ya BASATA kuhusu 'video' za Menina
0
October 11, 2019
Baraza la sanaa la Taifa (BASATA), limemuita msanii wa filamu nchini Menina Tz, ikiwa ni masaa machache tu, tangu zisambae video na picha zake zisizokuwa na maadili katika mitandao ya kijamii.
Akizungumza na EATV & EA Radio Digital, Katibu Mtendaji wa Baraza la sanaa la Taifa Godfrey Mngereza, amesema ni wazi wamemwita msanii huyo ili kuzungumza naye.
“Tumemwita na tumekubaliana tukutane leo, kuhusu kilichotokea kwenye mitandao na mengine tutajua hapo tutakapokutana naye, kuna aina mbili hadi yanatokea hayo inawezekana kutokujua athari za mitandao na wengine wanapokuwa kwenye mahusiano wanajisahau” amesema Mngereza.
Aidha amesisitiza umuhimu wa wasanii nchini kuzingatia Sheria na kanuni ziliwekwa na Baraza hilo.
“Sipendi sana niingie kwenye sheria au kanuni kwa sababu ukiangalia yaliyotokea yana pande nyingi sana na sisi sheria zetu ni kuzungumza nae kwanza na kumsikiliza ila kama Baraza cha kwanza ni kumwita kwa sababu anahusika kwenye kazi za sanaa” amesema Mngereza.
Mngereza ameongeza kuwa wao kama Baraza la Sanaa, hawawezi kutoa hukumu hadi uchunguzi utakapokamilika na kushauri watu kuheshimu faragha zao na kwamba masuala ya faragha yawe ya faragha, hakuna haja ya kujirekodi na kuviweka hadharani.
Tags