KENYA: Zaidi ya Wafugaji 2,000 Waiomba Serikali Kuwabadilishia Fedha Zisizotumika

KENYA: Zaidi ya wafugaji 2,000 waiomba serikali kuwabadilishia fedha zisizotumika
Zaidi ya wafugaji 2,000 wa kuhama hama nchini Kenya wamesalia noti za zamani za shilingi elfu moja ($10) ambayo haitumiki tena nchini humo.Wafugaji hao ambao wamekuwa wakilisha mifugo wao katika misitu ya Witu na Boni Pwani ya Kenya wanasema walishindwa kufika nyumbani kubadilisha noti hizo baada ya ”kushindwa kufikia muda wa mwisho wa Septemba 30 uliowekwa na Benki Kuu ya Kenya .”

Wafugaji hao sasa wanatoa wito kwa Benki Kuu ya Kenya kuwapa fursa ya kubadilisha noti hizo za zamani

Baadhi yao waliliambia Gazeti la Nation, kuwa walifahamishwa kwamba noti hiyo ya shilingi 1,000 haitumiki tena walipofika maeneo ya mjini na kujaribu kuitumia kununua bidhaa.

“Tulijaribu kulipia chakula katika mgahawa mmoja mjini Minjila, tukaambiwa pesa hiyo haitumikio tena. Karibu tukosane na mmiliki wa mgahawa huo lakini tulielezewa kilichojiri,” alisema Mohammed Barisa.

Bw Barisa pia aliongezea kuwa karibu wafugaji 2,000 bado wapo malishoni na hawana habari kuhusu mabadiliko yanayoendelea nchini.

Kundi la wafugaji liliondoka nyumbani mwezi Februari mwaka huu kutafutia mifugo yao malisho na maji na inasemekana hawakua na mawasiliano ya aina yoyote au ufahamu kuhusu mabadiliko ya sarafu ya shilingi elfu moja.

Wafugaji hao hao wameelezea hasara waliopata kutoka kwa wafanyibiashara walaghai walionunua mifugo yao kwa kutumia Noti hiyo ya zamani walipokua njiani kurejea nyumbani.

“Tuliwauza watu kadhaa kondoo na mbuzi na walitulipa kwa kutumia noti ya shilingi 1,000.

Tumesalia na karibu shilingi 200,000 ($2,000), na sasa tumearifiwa kuwa ni karatasi ambayo hakuna benki inaweza kukubali,”Ishmael Barako, mmoja wa wafugaji hao aliimbia gazeti hilo.

Wafugaji hao sasa wanatoa wito kwa Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Patrick Njoroge kuwapa nafasi ya kubadilisha noti hizo za zamani.

“Tupo katika makundi tofauti kutoka maeneo tofauti na kiongozi wetu anaweza kuthibitisha kila kitu kwa njia ya uwazi ili kutuokoa dhidi ya hasara inayotukodolea macho,”aliongeza Bw. Barako.

Kwa mujibu wa Shirika la kitaifa la kukabiliana na Ukame, zaidi ya wafugaji wa kuhama hama 5,000 waliripotiwa kuhamia maeneo ya Lamu na Tana Delta Pwani ya Kenya kutafutia mifugo wao malisho na maji.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad